Aliitaja Sekta ya Utalii Zanzibar kuwa imebarikiwa na mazingira
mazuri ya rasilmali mbali mbali zinazotoa nafasi pana kwa Miradi ya
Kitalii kama Hoteli pamoja na Usafiri wa Anga kuendelea kuwekezwa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa msisitizo huo wakati wa mazungumzo yake
na Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Mauritius Bwana Santaram Baboo
aliyeuongoza Ujumbe wa Viongozi Watano wa Sekta ya Utamaduni kutoka
Mauritius uliofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema Visiwa vya Mauritius vimepiga hatua kubwa kimaendeleo katika
Sekta ya Utalii ndani ya kipindi kifupi hatua ambayo Wawekezaji hao hao
wanaweza pia kufungua milango ya Uwekezaji hapa Zanzibar katika azma ya
kuendeleza ushirikiano wa pande hizo mbili zinazofanana Kiutamaduni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Mauritius
kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuwakaribisha
Wawekezaji wa Visiwa hivyo kwa kufunga mikataba ya uanzishwaji wa miradi
hiyo wakati wowote kuanzia sasa.
Mapema Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Visiwa vya Mauritius Bwana
Santaram Baboo alisema upo uhusiano mkubwa wa Kihistoria unaofanana kati
ya Zanzibar na Nchi yake hasa katika masuala ya Utamaduni pamoja na
uhifadhi wa urithi wa Kimataifa.
Bwana Baboo alisema Zanzibar kama ilivyo Mauritius kwa uzuri wake wa
maumbile katika rasilmali za Baharini inaweza kutumiwa na Wasanii mbali
mbali wa Kimataifa kurikodi Vipindi tofauti vinavyoweza Kuelimisha,
kufurahisha lakini pia Kuitangaza Zanzibar Kiutalii Ulimwenguni.
Waziri huyo wa Sanaa na Utamaduni wa Mauritius alisema mpango huo pia
unaweza kuinyanyua Zanzibar Kiuchumi kama ilivyofanikiwa Nchi yake
ambayo kwa sasa imekuwa ikipokea watalii Milioni 1.6 kwa mwaka wakati
Visiwa vyenyewe vina Idadi ya wakaazi Milioni 1.3.
Bwana Santaram Baboo alielezea kufurahishwa kwake na mazingira
mazuri ya uwekezaji yaliyopo Zanzibar kiasi kwamba mbali ya kurejea kwao
kushawishi Makampuni na Taasisi za Uwekezaji za Nchi hiyo lakini pia na
yeye binafsi ameshawishika kutaka kuwekeza katika miradi ya Hoteli.
Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Visiwa vya Mauritius Bwana Santaram
Baboo na Ujumbe wake umekuja Tanzania na Zanzibar kwa ziara maalum ya
kuangalia maeneo ya uwekezaji ambayo Nchi hiyo inaweza kuyatumia katika
kuanzisha miradi ya Kiuchumi itakayoendeleza uhusiano kati ya pande hizo
mbili.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
5/12/2016.
chanzo; zanzibar24.
Comments