Balozi Seif aifungulia Cuba milango ya uwekezaji Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wawekezaji na wananchi wa Jamuhuri ya Cuba wana nafasi nzuri ya kutumia  mlango wa uwekezaji uliofunguliwa na Zanzibar katika kuanzisha miradi mipya  kwenye Sekta ya Utalii hapa Nchini.
Alisema mpango huo ambao licha ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu  uliopo kati ya Zanzibar na Cuba tokea Uhuru wa Mataifa hayo Mawili lakini pia utaongeza ushirikiano wa  pande hizo zinazofanana katika Historia zake.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez  aliyefika kumuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa Nchini.
Alieleza kwamba  Cuba imekuwa mshirika mkubwa wa harakati za maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar hasa katika kusaidia Taaluma ya Sekta za Afya na Kilimo chini ya Muasisi wa Taifa hilo Marehemu Fidel Castro.
Balozi Seif  alisema  mafungamano hayo kwa sasa yanapaswa  kuelezwa nguvu zake katika Sekta ya Utalii inayoonekana kushamiri zaidi hivi sasa Ulimwenguni na kuleta mapato makubwa yanayochangia Mataifa  mbali mbali  ambayo tayari yamekwisha wekeza kwenye  miradi hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alimuomba Balozi Jorge Luis licha ya kumaliza muda wake wa  Kidiplomasia hapa Tanzania lakini bado ana nafasi ya kuisaidia Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika kuzitangaza Kiutalii kwa wawekezaji wa Nchi yake wakati atakaporejea nyumbani.
Aliishukuru Serikali ya Cuba kwa juhudi kubwa  iliyochukuwa katika kusaidia maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar  ambao katika maisha yao yote ya baadaye wataendelea kuzikumbuka juhudi hizo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba wataalamu  wengi wa Cuba  hasa wale wa Sekta ya Afya waliowahi kutoa Taaluma kwa vijana na  Wananchi tofauti wa Zanzibar  ni mfano halisi wa juhudi hizo.
Mapema Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez  alisema kwamba uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Cuba  utaendelea kama kawaida licha ya mabadiliko ya watendaji wanaosimamia uhusiano huo.
Balozi Lopez alimuhakikishia Balozi Seif  kuwa mrithi wa kuchukuwa nafasi yake anayetarajiwa kuingia Nchini Tanzania wakati  wowote  kuanzia sasa ni Mwanadiplomasia mzoefu  mwenye upeo wa  kuzifahamu Siasa na mazingira ya Mataifa ya Bara la Afrika.
Bwana  Lopez alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wazo lake la kumuomba kuitangaza Zanzibar atakaporejea nyumbani  kwake atalifanyia kazi ipasavyo ili kuweka kumbu kumbu nzuri wa uwepo wake wa kazi  Nchini Tanzania.
Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Bwana Jorge Luis Lopez  ambae mapema alikutana kwa Mazungumzo na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Zubeir Ali Maulidi anarejea Nyumbani baada ya kumaliza muda wake wa kazi wa Miaka Minne hapa Tanzania.
chanzo;zanzibar24.

Comments