Mwakilishi wa UNICEF katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Maniza
Zaman aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na
mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein.
Mwakilishi huyo wa UNICEF hapa nchini alieleza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika
kuwahudumia watoto sambamba na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi
ikiwemo kupata elimu na afya bora.
Alieleza kuwa Shirika hilo linathamini juhudi hizo na limeweza
kushuhudia mafanikio na mabadiliko makubwa katika sekta za maendeleo
hatua ambazo zimewawezesha watoto wa Zanzibar na wao kuweza kupata haki
zao za msingi pamoja na mahitaji yao muhimu ya kimaisha.
Bi Zaman alizipongeza hatua za Serikali ya Mapinduzi za kujenga
majengo mapya yatakayowahudumia wanawake na watoto katika hospitali ya
Manzi Mmoja na ujenzi wa hospitali mpya ya Abdalla Mazee ni miongoni mwa
mafanikio katika sekta ya afya ambayo watoto nao watafaidika.
Vilevile, Mwakilishi huyo alimpongeza Dk. Shein kwa juhudi zake kubwa
anazozichukua katika kupiga vita vitendo Ukatili na udhalilishaji wa
wanawake na watoto kupitia Kampeni aliyoianza mnamo mwaka 2014, kwa
ajili ya kukomesha vitendo hivyo.
Alieleza kuwa hatua za Serikali katika kuhakikisha vifo vya akinamama
na watoto vinapungua hapa Zanzibar sambamba na kukabiliana na tatizo la
mtapiamlo kwa watoto navyo vimepata mafanikio ambapo UNICEF pia,
imeahidi kuendelea kuziunga mkono juhudi hizo.
Mwakilishi huyo alieleza kuwa UNICEF tayari imeshaanzisha programu
mbali mbali mpya pamoja na kuziendeleza zile za zamani katika suala zima
la kuwahudumia watoto na kueleza azma yake ya kwenda ngazi za chini
zaidi katika jamii kwa kushirikiana na serikali katika kutatua
changamoto zinazowakabili watoto.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein kwa upande wake amelipongeza Shirika la UNICEF kwa juhudi
zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kuahidi kuimarisha uhusiano
na mashirikiano yaliopo.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Shirika la UNICEF lina
historia kubwa na mashirikiano kati yake na Zanzibar ikiwa ni pamoja na
kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo sekta ya afya, elimu sambamba na
kuimarisha ustawi wa akinamama na watoto.
Dk. Shein alisema kuwa Shirika hilo limeweza kutoa misaada yake
mbalimbali na kuweza kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya afya kwa
kushirikiana na Shrika la Afya Duniani (WHO).
Aidha, Dk. Shein amesema kuwa licha ya changamoto kadhaa
zinazowakabili watoto katika Bara la Afrika lakini bado Shirika hilo
limeendelea kutoa ushirikiano wake na misaada mbali mbali kwa watoto
walio ndani ya nchi za bara hilo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza juhudi zilizochukuliwa katika
kupambana na vifo vya akinamama na watoto, ambapo Zanzibar imepiga hatua
kubwa hasa pale ilipoanzisha mapambano dhidi ya Malaria jambo ambalo
limefanikiwa.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo, kutoa pongezi kwa Shirika hilo kwa
kuungana na Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa (UN) yenye Ofisi zake
hapa Zanzibar kuunda ‘One UN’ iliozipelekea ofisi hizo kukaa katika
jengo moja na kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kuzisimamia vyema, Sera, Kanuni na Sheria zinazowahusu watoto katika
kupata haki zao za msingi na huduma za kijamii.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
chanzo; zanzibar24.
Comments