Samia acharuka Mwanza.

MAKAMU wa Rais wa Samia Suluhu Hassan ametoa muda wa mwezi mmoja kuanzia jana kwa watendaji na viongozi waandamizi wa wilaya ya Ilemela kuhamia kwenye wilaya hiyo na kuacha tabia ya kukaa kwenye wilaya nyingine kwa kisingizio cha kukosa nyumba za serikali.

Makamu wa Rais alitoa agizo hilo katika hotuba yake kwa wananchi na watendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela waliojitokeza katika hafla ya uzinduzi jengo la utawala la manispaa hiyo na kukabidhi madawati 1,074 yaliyotolewa na ofisi ya Bunge.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mawasiliano ya Makamu wa Rais ilisema, Samia amewataka watendaji hao kuwa karibu na maeneo yao ya kazi ili waweze kuwa karibu na wananchi na kuwasaidia kutatua kero na matatizo yanayowakabili kwa haraka.

Akiwa katika wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza wakati anaweka jiwe la msingi katika mradi wa ukarabati wa machinjio ya Nyakato jijini Mwanza, Makamu wa Rais aliuagiza uongozi wa jiji la Mwanza kusimamia kikamilifu mradi wa ukarabati wa machinjio ya Nyakato na kwamba watendaji watakaobainika kuhujumu mradi ambao utagharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo katika hotuba yake kwa wananchi na watendaji wa jiji la Mwanza waliohudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ukarabati wa machinjio ya Nyakato unaohusisha uboreshaji wa jengo la machinjio, tangi la kuhifadhi maji, ujenzi wa vyumba vya baridi vya kuhifadhi nyama na ujenzi wa mtambo wa kutibu majitaka yanayotoka kwenye machinjio hiyo.

Makamu wa Rais pia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuhakikisha anasimamia uundaji wa menejimenti ya machinjio hiyo ambayo itaboresha utendaji kazi wa machinjio hiyo.

Kuhusu ukusanyaji wa kodi, Makamu wa Rais aliwahimiza watendaji wa halmashauri zote za mkoa wa Mwanza kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa njia ya kielektroniki kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya fedha ambavyo vitasaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi mkoani humo.

Samia alitoa mwito kwa wananchi kuhakikisha wanadai risiti wanaponunua bidhaa mbalimbali, kwani kufanya hiyo kutasaidia kuongeza mapato ambayo yataelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Katika mkutano wake wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani Mwanza, Makamu wa Rais Samia alisisitiza viongozi na watendaji wa mkoa wa Mwanza kufanya kazi kwa bidii katika kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za umma.

Alionya kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitasika kuwachukulia hatua kali viongozi na watendaji ambao watakwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma kwenye maeneo yao ya kazi.

Aliwataka viongozi wa mkoa wa Mwanza kusimamia kikamilifu kulinda hali ya amani na utulivu na wachukue hatua kali kwa watu wanaotaka kuharibu amani ya nchi.

Makamu wa Rais amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani Mwanza kwa kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya mbalimbali ya maendeleo katika wilaya za Ilemela, Misungwi, Kwimba, Magu na Nyamagana.

chanzo;habarileo.

Comments