Mhadhiri wa Chuo cha Takwimu cha Afrika Mashariki, Dk. Camillus
Kassala amesema sababu inayochangia ukuaji wa pato la taifa kutowiana na
hali ya uchumi wa wananchi wengi ni mfumo mbovu wa ugawaji wa pato
hilo.
Dk. kassala ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa
maadhimisho ya siku ya takwimu barani Afrika inayoadhimishwa Novemba 18
kila mwaka.
“Kumekuwepo na mkanganyiko juu ya uwiano wa hali ya kiuchumi ya
wananchi na ukuaji wa pato la taifa, itambulike kuwa, pato la kila
mwananchi hugawanywa kwa mfumo wa wastani, inachukuliwa pato la taifa
linagawaiwa kwa idadi ya wananchi waliopo,” amesema na kuongeza.
“Tatizo linapo anza ni pale serikali inapoligawa, kwamba huligawa
maeneo gani na je hayo maeneo hugusa wananchi wengi? Mfano, hugawa kwa
njia ya mshahara hivyo wasioajiriwa hawapati, hugawiwa katika mifuko ya
hifadhi ya jamii na kwamba wasiokuwepo hawapati gawiwo kwa usawa.”
Amesema kuwa “Mfumo wa ugawaji wa pato la taifa bado una mapungufu
ndio maana wananchi wengi wanalalamika kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi
haushuki kwao na hawafaidiki na pato la taifa ilhali wanakatwa kodi
inayokwenda katika pato hilo.”
Kwa mujibu wa takwimu iliyotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) inaonyesha kuwa katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka
huu pato la taifa limeendelea kukua kwa kasi ya asilimia 7.9
ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2015.
Dk. Kassala ameishauri serikali kuwa na takwimu sahihi hususan za
wananchi wake na pato la taifa ili kuona namna ya kugawa pato hilo kwa
usawa na kufikia wananchi wa kada zote.
chanzo; zanzibar24.
Comments