Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano ya mwaka 2004, ni kosa la jinai kughushi vyeti.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu Dar es Salaam mwishoni mwa wiki,
Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi, alisema mpaka sasa maofisa wa
baraza hilo waliosambazwa mikoani kufanya uhakiki huo, wengi wao
wamerejea na wachache waliobaki wanakamilisha kazi hiyo ili warejee Dar
es Salaam.
“Ni kama mchakato wa uhakiki uko katika hatua za mwisho na kinachofanyika sasa ni kufanya majumuisho.
Siwezi kusema lini hasa tutamaliza, lakini kazi kubwa tumemaliza na kinachofanyika sasa ni majumuisho,” alisema Nchimbi.
Alisema utaratibu wa uhakiki huo wa vyeti ulianza rasmi Oktoba 10 na
ulitarajiwa kukamilika Novemba 14, mwaka huu. Hata hivyo, alisema baada
ya uhakiki huo wa vyeti, baraza hilo litawasilisha mrejesho wa matokeo
ya uhakiki huo kwa taasisi husika zilizowasilisha vyeti vya watumishi
wake kwa hatua zaidi dhidi ya watumishi watakaobainika kufanya
udanganyifu.
“Sisi tunafanya uchambuzi wa vyeti hivi tulivyoletewa na taasisi
mbalimbali kwa ajili ya kuvihakiki, baada ya hapo tutatoa mrejesho kwa
taasisi husika kuwa kati ya vyeti ilivyotuletea vingapi ni vya kughushi
na taasisi hiyo ndio itakayochukua hatua,” alisema.
Hata hivyo, alifafanua kuwa kwa mujibu wa utaratibu wa Necta, mtu
akifanya udanganyifu wa vyeti kwa kughushi au kutumia cheti kimoja kwa
watu wawili, baraza hilo lina mamlaka ya kuwashtaki wahusika ikiwa ni
pamoja na kumnyang’anya cheti mwenye cheti.
Alisema vyeti vyote vya kidato cha nne na cha sita vinavyotolewa kwa
wahitimu ni mali ya Necta, hivyo endapo mtu akivitumia kinyume na
inavyotakiwa baraza hilo lina mamlaka ya kumnyang’anya mhusika cheti
hicho na kumshtaki.
Hivi karibuni, serikali ilitangaza rasmi kuanza kampeni ya
kuwashughulikia na kuwaondoa katika utumishi wa umma watumishi wote
walioajiriwa katika sekta hiyo wakitumia vyeti bandia.
Kutokana na kuanza kampeni hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano iliwataka
watumishi hao waanze kujitathmini na kuanza kujiondoa wenyewe kabla ya
kufikiwa na mabadiliko makubwa ya kusafisha sekta ya elimu na utumishi
wa umma yanayokuja nchini.
Tayari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Angella Kairuki ameiagiza Idara ya Usimamizi wa
Rasilimaliwatu (Utumishi) kuwachukulia hatua stahiki watumishi
watakaobainika kutumia vyeti visivyo vyao ili kupata ajira serikalini.
Naye Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu
(Utumishi), Leonard Mchau alisema ni kosa la jinai kughushi vyeti kwa
lengo la kujipatia kazi, hivyo endapo mtu atagundulika ameghushi vyeti
atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
Hata hivyo, tayari kuna baadhi ya taasisi zimebainika kuwa na
watumishi walioghushi vyeti ikiwemo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma ambayo ilihakiki watumishi 704 na kati yao 219
waligundulika kuwa waliajiriwa kwa vyeti vya kughushi.
chanzo;habarileo.
Comments