Gari la zimamoto kuwa moja ya sharti la kuwa halmashauri.

Waziri Mkuu, Kassim MajaliwaSERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa moja ya sifa za halmashauri nchini ni kuwa na gari la zimamoto ili kukabiliana na moto unaojitokeza na kusababisha hasara kubwa kwa wananchi pamoja na miundombinu ya umma.

Hayo yalisemwa Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipotembelea kiwanda cha Equator Suma JKT kinachojihusisha na uunganishaji magari ya zimamoto na matrekta.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwa sasa kumekuwa na matukio mengi ya moto na kusababisha hasara kubwa na majengo au vitu mbalimbali vimekuwa vikiteketea kabisa kutokana na kukosa magari hayo ambapo yangekuwepo angalau yangesaidia kupunguza uharibifu.

“Kutokana na kampuni hii kuja na teknolojia ya kisasa ya kuunganisha magari ya zimamoto moja ya sifa za halmashauri ni kuwa na gari la zimamoto ambalo litaweza kuwahi kuokoa vitu vinavyoungua ambapo zamani gharama za zimamoto zilikuwa ni kubwa zinafikia hadi milioni 500 kwa gari moja hivyo zilishindwa kununua,” alisema Majaliwa.

Alisema mara uzalishaji utakapoanza mwakani magari haya yatashuka bei kwani gharama itakuwa ni ndogo sana na halmashauri zitaokoa majengo ambayo yamekuwa yakikumbwa na moto mara kwa mara ikiwa ni pamoja na shule za sekondari na majengo ya umma.

Kwa upande wa matrekta, alisema asilimia 90 ya Watanzania ni wakulima hivyo uanzishwaji wa kiwanda hicho kutasaidia upatikanaji wa zana bora za kisasa za kilimo na matrekta hayo yatapatikana kwa bei nafuu.

Awali, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Equator Suma JKT, Kapteni Farijala Mkojera akisoma risala ya kiwanda hicho, alisema ujenzi wa kiwanda hicho ulianza mwaka 2011 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na kuanza uzalishaji Januari mwakani.

Mkojera alisema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 80 ya ujenzi na gharama hadi sasa ni ziadi ya Sh bilioni moja na kikikamilika kitagharimu zaidi ya Sh bilioni mbili kitakuwa na uwezo wa kuzalisha magari 100 na matrekta 3,000 kwa mwaka.

chanzo;habarileo.

Comments