WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameunga mkono marekebisho ya Katiba
ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa ajili ya kumpa uwezo Rais kuteua wajumbe
wa Baraza bila ya kushauriana na kiongozi wa upinzani huku wakitaka
marekebisho mengine zaidi kwa lengo la kuleta ufanisi.
Mwakilishi wa Jimbo la Shauri Moyo, Hamza Hassan Juma alisema wakati
umefika sasa kwa Katiba ya Zanzibar izingatie demokrasia ya mfumo wa
vyama vingi kwa vitendo na kuacha kuweka kipaumbele kwa vyama vya CCM na
CUF.
Alisema athari za kuvishirikisha vyama hivyo, ikiwemo katika Katiba
imeanza kuonekana ambapo mwaka jana viongozi wa CUF walisusia Baraza la
Wawakilishi wakati wa kupitisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2016/2017.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Chaani, Nasir Abdulatif Jussa (CCM)
alisema marekebisho yatakayopitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
yatampa uwezo mkubwa Rais wa Zanzibar sasa kuchagua wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi bila ya kupata ushauri kutoka kwa mtu yeyote.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Said Hassan Mzee alisema marekebisho hayo ni muhimu ambayo yataondoa
masharti na kumpa uwezo Rais kushauriana na kiongozi wa upinzani ambaye
kwa sasa hayupo.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipitisha muswada huo wa
Marekebisho ya 11 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo sasa
yatampa nafasi Rais wa Zanzibar kuchagua wajumbe wawili wa Baraza la
Wawakilishi katika nafasi 10 bila ya kushauriana na kiongozi wa upinzani
ambaye katika muundo wa Baraza la Wawakilishi la sasa hayupo.
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa sasa wajumbe wake wote wanatoka
CCM baada ya kushinda majimbo yote ya Unguja na Pemba kufuatia CUF
kususa uchaguzi wa marudio.
chanzo;habarileo.
Comments