Watakaoiba vyuma vya bustani Dar kulipa 10 zaidi.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema mtu yeyote atakayebainika kuiba au kuharibu vyuma vilivyowekwa katika bustani za pembezoni mwa barabara za mkoa huo atalazimika kununua vyuma 10 kama fidia.
 
Makonda alitahadharisha hivyo jijini humo wakati alipofanya ziara wilayani Kinondoni kujionea hali ilivyo katika bustani mbalimbali zilizowekewa uzio wa vyuma. Ukaguzi wa bustani hizo ni maandalizi kuelekea kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Mti Wangu itakayofanyika Oktoba mosi.

Alisema lengo la Serikali ni kuona jiji hilo linakuwa na muonekano wa kuvutia na kwamba hatamvumilia yeyote atakayeiba vyuma hivyo na atakayeharibu mazingira.

“Kuna watu hawajazoea kuona mambo mazuri, tunatengeneza ili kupendezesha jiji halafu wao wanawaza kuiba vyuma vya bustani na kuharibu mazingira. Atakayekamatwa atalipa vyuma 10 kwa kila chuma alichokiiba au kuharibu,”Makonda alisema.

Aidha, alisema baada ya kukamilisha kutengeneza bustani hiyo, watalazimika kuweka taa pamoja na nyaya za shoti ili kuzuia wananchi watakaotaka kufanya uharibifu.

Pia, alisema bustani hizo zitakuwa na maji safi kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (Dawasco) ambayo yatatumika kumwagilia kuliko kusubiri kipindi cha mvua pekee au kupeleka maji kwa kutumia magari.

Makonda pia aliwataka wakazi wa jiji hilo wenye kampuni pembezoni mwa barabara kuchukua jukumu la kuzitunza bustani hizo na watapewa mita za maji kila mmoja, ikiwa ni pamoja na jukumu la kuzisimamia ili kuhakikisha zinabaki katika muonekano mzuri.

“Lengo ni moja na ushiriki wa kampuni ni muhimu, kampuni zote zitapewa utaratibu ikiwemo kupewa mita za maji na kuhakikisha bustani iliyo mbele ya ofisi ya kila kampuni inakuwa na muonekano mzuri,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Makonda alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi kuwatafutia eneo wafanyabiashara wanaouza bidhaa pembezoni mwa barabara katika eneo la Moroco kwa kuwa eneo wanalolitumia kwa sasa si halali kwa biashara.

Kwa upande wake, Hapi alisema wilaya hiyo itapanda miti zaidi ya 5000 na kwamba kwa sasa wanaendelea kufunga miundombinu ya maji na kuchimba mashimo kwa ajili ya kupanda miti hiyo.

chanzo;habarileo.

Comments