WAKILI wa Kujitegemea Godwin Muganyizi (44) amepandishwa kizimbani
akikabiliwa na mashitaka ya kughushi mhuri wa benki ya NMB, kuonesha
amri ya kukazia hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar es Salaam imepokelewa na benki hiyo.
Mbali na Muganyizi washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Maseke
Zenge (50), Mhasibu Augustine Mrema (55) na Ofisa wa Kampuni ya udalali
ya Unyangala Auction Mart, Ahadik Kambona.
Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga alidai mbele ya Hakimu Mkazi
Emmillius Mchauru kuwa katika tarehe isiyofahamika washtakiwa hao
walikula njama ya kutenda kosa.
Aliendelea kudai kuwa, Juni 19, 2014, wakiwa Dar es Salaam kwa nia ya
udanganyifu, washtakiwa walighushi mhuri wa benki hiyo kuonesha amri ya
kukazia hukumu imepokelewa na benki hiyo huku wakijua si kweli.
Katika shitaka la tatu inadaiwa, siku hiyo, washtakiwa walighushi
saini ya Ofisa wa benki hiyo kuonesha ametia saini kupokea kikazia
hukumu jambo ambalo si kweli.
Aidha, inadaiwa Agosti 22, 2014 wakiwa kwenye jengo la NMB katika
mitaa ya Azikiwe na Jamhuri waliwasilisha kwa Ofisa wa Sheria NMB
nyaraka hiyo kuonesha imetolewa na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya
Kisutu huku wakijua si kweli.
Katika mashitaka mengine inadaiwa, washtakiwa wakiwa katika jengo
hilo kwa njia ya udanganyifu walijaribu kujipatia Sh milioni 51,640,000
kutoka kwenye benki hiyo, baada ya kudanganya kuwa hukumu ya benki hiyo
inapaswa kulipa fedha hizo zilizoandikwa kwenye kikazia hukumu.
Washtakiwa walikana kuhusika na makosa hayo na Wakili Katuga alidai
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine
ya kutajwa.
Washtakiwa waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kila
mmoja kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh milioni 10. Kesi
hiyo itatajwa tena Oktoba 5, mwaka huu.
chanzo;habarileo.
Comments