KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema utashi wa
kisiasa, matumizi ya Pato la Taifa na matumizi ya fursa mbalimbali
unaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi ya mfano katika uboreshaji na
upatikanaji wa elimu kwa wote.
Ban Ki-moon aliyasema hayo juzi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ripoti
ya Kamisheni ya Kimataifa kuhusu, “Kizazi kinachojifunza: Uwekezaji
katika elimu kwa dunia inayobadilika” iliyofanyika katika Makao Makuu ya
UN na kuhudhuriwa karibu na makamishna wote wanaounda tume hiyo akiwamo
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
Tume hiyo ambayo ipo chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu mstaafu wa
Uingereza ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa Katika Mkuu wa Umoja wa
Mataifa kuhusu Elimu, David Cameroon inawahusisha pia baadhi ya marais
waliopo madakarani, mawaziri wakuu waliopo madarakani na waliostaafu.
Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunia, Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO),
wawekezaji wakubwa akiwamo tajiri namba moja Afrika, Aliko Dangote,
taasisi za utafiti, wataalamu wa masuala ya fedha, asasi za kijamii na
makundi ya vijana wakiwamo wanafunzi.
“Uzoefu wa nchi kama Tanzania, Vietnam na nchi yangu mwenyewe Korea,
unaonesha kwamba pale ambapo pana utashi wa kisiasa, ukijumuishwa na
uwepo wa fursa na raslimali fedha kuna kitu kinachoweza kufanyika katika
elimu,” alisema Ki-moon.
Na kutokana na uzoefu wa nchi kama Tanzania na nyinginezo, mkuu huyo
wa Umoja wa Mataifa alisema Jumuiya ya Kimataifa ni lazima iwe tayari
kuzisaidia kwa mitaji nchi ambazo zimeamua na kujituma katika kuifanyia
mageuzi mifumo yake ya elimu na kujipati matokeo yanayoridhisha.
Akichangia majadiliano ya uzinduzi wa ripoti hiyo, Rais mstaafu
Kikwete kama mmoja wa makamishna na ambaye pia aliongoza majadiliano
kuhusu kipengele cha tatu cha mapendekezo ya ripoti hiyo kuhusu
ujumuishi katika elimu, alisema, “Mafanikio ya elimu lazima yamfikie
kila mmoja wakiwamo wale wanaoishi katika mazingira magugumu na
wanaobaguliwa wakiwamo wasichana.”
Aliongeza kuwa bahati mbaya leo hii Afrika Kusini mwa Jangwa la
Sahara, msichana mmoja kati ya 20 wanaoishi katika maeneo ya umaskini
ndiyo walio katika hatua za kumaliza elimu ya msingi, na kwamba
takribani watoto milioni 75 ambao wamo katika umri wa kwenda shule
wanakabiliwa kila siku na hatari moja ama nyingine.
chanzo;mpekuziblog.
Comments