WAKATI ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma umefikia asilimia 100,
kumekuwa na na ongezeko la ndege zinazotua kila siku kutoka ndege tatu
hadi kufikia tisa.
Akizungumza wakati wa mahojiano jana, Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha
Dodoma, Julius Mlungwana alisema kukamilika kwa ukarabati huo
kutawezesha mashirika mengi ya ndege kuanza safari zake kuja Dodoma na
hivyo kupunguza gharama za nauli.
Mlungwana alisema ukarabati huo umekamilika Septemba 2, mwaka huu na
kina uwezo wa kuhudumua ndege zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 90.
“Uwanja umekamilika kwa asilimia 100 kwa lengo la msingi na
kilichobakia ni kuweka alama tu,” alisema meneja huyo na kuongeza kuwa
kwenye usafiri wa anga kuna wadau wanaotumia kiwanja wakiwemo
wafanyabiashara, wafanyakazi wa umma, mawakala wa utalii, taasisi za
kimataifa na serikali, taasisi zisizo za kiserikali na wananchi.
“Hao wote wanatumia usafiri wa anga kilio chao kikubwa, nauli za
ndege ni kubwa,” alisema na kuongeza kuwa kilio cha wadau kwenye usafiri
wa anga ni gharama kubwa za usafiri kutokana na kuwepo kwa ndege mbili
zilizo kwenye ratiba ya usafiri ambazo ni Auric Air na Flight Link
ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 13 kila moja.
“Pia kuna ndege zisizo na ratiba na za viongozi ambazo hazipo kwenye
mpangilio pamoja na mashirika ya kimataifa ambao wamekuwa wakitumia
ndege za kukodi,” alisema.
Naye Meneja Mradi wa Upanuzi wa uwanja huo kutoka Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege Tanzania (TAA), Mbila Mdemu alisema mara ya mwisho ukarabati
wa uwanja huo ulifanyika mwaka 1976, na 2005 ulifanyika upembuzi
yakinifu kwa ajili ya ukarabati, lakini upatikanaji wa fedha umekuwa ni
kikwazo na usanifu ukaishia kwenye ukarabati.
Alisema kutokana na agizo la Rais John Magufuli kuhamia Dodoma, uwanja ulianza kufanyiwa ukarabati.
Awali ujenzi ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi sita na kuliwekwa
malengo mawili ambapo ilitakiwa hadi Julai 20, mwaka huu kiwanja kiwe na
uwezo wa kuhudumua ndege zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 70 na 90.
Pia hadi Agosti 31, mwaka huu kazi za msingi zote ziwe zimekamilika na
kazi zote zimefanikiwa kukamilika.
chanzo;habarileo.
Comments