MBUNGE wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka amesema amekabidhiwa
tuzo nchini Marekani, lakini amekataa kupokea fedha zinazoambatana na
tuzo hiyo ambazo ni Dola za Marekani 100,000 (zaidi ya Sh milioni 200)
kutokana na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo iliwahi kumtia
matatani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Profesa
Tibaijuka alisema tuzo hiyo ni ya Maendeleo Endelevu ya Mwana wa Mfalme
Khalifa bin Salman Al Khalifa wa Bahrain ambazo zilitolewa katika Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani usiku wa Septemba 23,
mwaka huu.
“Tuzo hizi zinaambatana na fedha, lakini sikuichukua kwa sababu ya
yaliyonikuta hapa, niliwaambia naacha mezani nyie mtaamua cha kufanya
maana kwa sheria ya nyumbani hatuna sheria ya kupokea zawadi,” alisema
Profesa Tibaijuka ambaye mwaka jana aliingia matatani baada ya kupewa Sh
bilioni 167 zilizotokana na mgawo wa mfanyabiashara James Rugemarila
kutokana na fedha za akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Alisema ameshinda tuzo hiyo ikiwa ni kutambua mchango wake katika
kuhamasisha maendeleo duniani na sherehe za utoaji wa tuzo hizo
ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali duniani wakiwemo mabalozi na
mawaziri. Tuzo hizo hutolewa kila baada ya miaka miwili ambapo washiriki
wakuu huwa ni wale waliowahi kufanya kazi Umoja wa Mataifa.
Profesa Tibaijuka aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat).
chanzo;habarileo.
Comments