SMZ kuboresha maslahi ya waandishi.


 Image result for shein

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, amesema serikali itafanya kila linalowezekana kuhakikisha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya wafanyakazi wa vyombo vya habari vya serikali yanaimarishwa ili kurejesha hadhi ya taasisi hizo.

Dk Shein ambaye alitembelea redio na gazeti la Zanzibar Leo na kufanya mahojiano maalumu na Shirika la Habari na Utangazaji Zanzibar (ZBC), alisema ameridhishwa na utendaji wa kazi wa viongozi na wafanyakazi wa vyombo, ambao wamekuwa wakijitahidi kufanya kazi vizuri, licha ya changamoto wanazokabiliana nazo.

Alisema serikali imedhamiria kufanyia marekebisho makubwa ZBC na vyombo vyote vya habari vya serikali sio tu kwa kuinua viwango vya mishahara ya wafanyakazi, lakini pia kutoa tuzo maalumu kila inapohitajika kwa wafanyakazi watakaofanya kazi vizuri ili kuinua ari na motisha ya kazi.

Katika hatua za awali za kuziimarisha taasisi za vyombo vya habari vya serikali, alisema serikali imeshatoa agizo kuitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, kuandaa posho maalumu kwa wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Akizungumzia baadhi ya wafanyakazi ambao wameondoka kwenye vyombo vya habari vya serikali kutokana na maslahi duni na mazingira yasiyoridhisha, alisema ana matumaini makubwa kwamba wengi wao watarejea siku zijazo kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwenye taasisi mbalimbali.

Rais wa Zanzibar kuhusu Zanzibar Leo alisema, serikali imeshanunua mitambo mipya ya kisasa ya uchapishaji ambayo itatumika pia kuchapishia gazeti hilo badala ya kuchapishwa nje ya Zanzibar, jambo linalosababisha mlundikano mkubwa wa deni la gharama za uchapishaji.

Jumamosi iliyopita, Rais wa Zanzibar alikutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Uongozi wa Shirika la Habari na Utangazaji Zanzibar (ZBC) na wa Zanzibar Leo, kuzungumzia mkakati wa kusaidia kuimarisha matangazo ya redio na Tv katika Shirika la Habari na Utangazaji Zanzibar (ZBC).

chanzo;habarileo.

Comments