WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imezifuta
shule za awali, msingi na sekondari nchini ambazo hazijasajiliwa zaidi
ya 40 kuanzia Julai mwaka jana.
Awali kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, waligundua kuwepo kwa
shule 35 zisizosajiliwa na kuzifuta, jambo lililofanya kutangaza shule
zote ambazo hazijasajiliwa kujisalimisha ili kusajiliwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa Shule katika wizara hiyo, Khadija
Mcheka alisema Mei mwaka huu baada kuzipa miezi miwili shule ambazo
hazijasajiliwa kufanya hivyo, walizifungia shule nyingine 12.
Mcheka alisema shule zinaweza kufutwa kwa sababu mbili zikiwamo
zilizosajiliwa, lakini zikakiuka vigezo ambazo zikitimiza vigezo
zinaweza kuomba upya usajili na kupewa.
“Lakini aina ya pili ni zile ambazo hazijasajiliwa na zinaendeshwa
kinyume cha sheria ambazo nazo zikifuata taratibu zikatimiza vigezo
zinaweza kupewa usajili,” alifafanua Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa
Shule.
Alisema katika kipindi hicho mpaka Agosti mwaka huu baada ya tangazo
la kuwataka kusajiliwa shule za awali nne, zile za awali na msingi 105
na sekondari 19, walifika wizarani kwa ajili ya kupata taratibu za
usajili ambapo zipo zilizosajiliwa na nyingine kupewa vibali.
Alisema katika usajili, kuna wapo waliokidhi viwango na wengine
waliopatiwa maelekezo na kupatiwa vibali vya kutumia majengo yaliyopo
huku wengine wakipewa vibali vya kujenga majengo ya shule kabla ya
kupata usajili.
Alisema kwa shule walizozifungia, waliwaandikia barua za kuwafungia
na kuwataka kuhakikisha wanawatawanya wanafunzi katika shule
zilizosajiliwa kwa gharama zao bila kuwaathiri wanafunzi.
Alitaja shule zilizofungiwa kwa kuendesha shughuli zake bila usajili
kuwa ni shule za awali na msingi za Must Lead ya mkoa wa Pwani, na za
mkoa wa Dar es Salaam ni Brainstorm, Pax, Lassana, Grace, Rose Land,
Julius Raymod, St Thomas, Mary Mother of Mercy, Noble Sinkonde,
Immaculate Heart of Mary, St Columba, Corner stone, Dancraig, Mwalimu
Edward Kalunga, Edson Mwidunda, Gisela, Kingstar, St Columba awali,
Bilal Muslim, Thado, Hocet , Elishadai, Lawrance Citizen, Comrade, Dar
Elite Preparatory na Golden Hill Academy na Hekima.
Nyingine ni Pwani Islamic, St Kizito na Rwazi Encysloped za Kagera,
Dancraig na Qunu za Pwani, Hellen’s ya Njombe, Joseph ya Arusha,
Samandito na Maguzu za Geita. Alizitaja shule za Sekondari zilizofungiwa
kwa sababu hiyo kuwa ni Hananasif, Elu, Hocet, Safina za Dar es Salaam
na Namnyaki ya Iringa.
Aidha, Shule ya Fountain Gate ya jijini Dar es Salaam imefungiwa kwa kuendesha bweni bila kibali.
“Baada ya kutoa tangazo kutokana na kubaini kuwapo shule nyingi
zisizosajiliwa, wapo waliojitokeza na nyingine tumezifungia kutokana na
kutokidhi viwango vya usajili lakini pia tunaamini wapo waliojificha
wakiendelea kutoa huduma,” alisema Mcheka na kuwaagiza wakaguzi katika
kanda na wilaya, kufanya ukaguzi na kutoa taarifa kwa zile ambazo
hazijafungiwa na ikithibitika hazijasajiliwa, kuzifungia mara moja.
Alisema utaratibu uliopo kwa kuhakikisha shule zote zinasajiliwa
kulingana na viwango stahili kwa lengo la kutoa elimu bora ni wakaguzi
wa kanda, mikoa na wilaya kwa kushauriana na waratibu wa elimu katika
kata, kuhakikisha shule yoyote inayochomoza, wanaifuatilia na kuwapa
ushauri wa kufuata taratibu za usajili kwa kukidhi viwango stahili.
Alisema wamekuwa wakigundua kuwapo kwa shule, ambazo hazijasajiliwa
kutokana na wakati wa mitihani idadi ya wanafunzi inazidi tofauti na
walivyosajiliwa na kubainika kuwa wapo waliokuwa wakisoma katika shule,
ambazo hazijasajiliwa wanawapeleka katika shule zilizosajiliwa.
“Kuna wenye shule ambazo hazijasajiliwa wakati wa mitihani wanakuja
kuomba wanafunzi kufanya mitihani hivyo kuleta usumbufu wa kuwatawanya
kwenye shule zilizosajiliwa na kwenda kuwakagua ili kuweza kusajiliwa,”
alifafanua.
Msajili huyo alisema madhara yanayotokana na mwanafunzi kusoma shule
ambazo hazijasajiliwa ni pamoja na haitajulikana mtoto anachosoma kwani
haitajulikana mitaala wanayotumia kutokana na kukosa usajili, hivyo
kushindwa kufanya mitihani. Pia mazingira ya shule na mpangilio wake,
haitaendana na matakwa ya serikali ya kutoa elimu bora kwani mmiliki
atafanya kile anachotaka.
Mei mwaka huu, wizara hiyo ilizipa miezi miwili hadi Julai 30, mwaka
huu kuhakikisha shule zote ambazo hazijasajiliwa zinajisajili kabla ya
serikali kuzifunga.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo
ya Ufundi, Dk Leonard Akwilapo alisema ifikapo Julai 30, mwaka huu,
mmiliki wa shule itakayobainika kutosajiliwa ikiwemo zitakazokosa vigezo
vya kusajiliwa, atapaswa kuhamisha wanafunzi waliopo kwa gharama zake.
Alipoulizwa ni shule ngapi ambazo zinajiendesha bila kusajiliwa,
Kaimu Mkurugenzi Mcheka alisema tatizo kubwa lipo kwa shule za awali na
msingi.
chano;habarileo.
Comments