MKUU wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu amesema tathimini inayoendelea
kuhusu athari za tetemeko la ardhi lililotokea mkoani humo Septemba 10,
mwaka huu, imebaini kuwa nyumba 2,072 zimeanguka kabisa, nyumba 14,525
zina nyufa kubwa na hazipaswi kuishi watu na nyumba zaidi ya 9,000
zinahitaji kufanyiwa marekebisho.
Aidha, imefahamika kuwa Sh bilioni tisa zinahitajika ili kujenga na
kurekebisha makazi ya wananchi wa Kagera yaliyoathiriwa na tetemeko la
ardhi kubwa.
Kijuu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Mkoa alisema
hayo wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Maafa Kitaifa katika Ofisi ya
Waziri Mkuu ikiongozwa na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Ajira na wenye
Ulemavu, Jenista Mhagama ili kujua maendeleo ya tathimini inayoendelea.
“Mpaka sasa tathimini imebainika nyumba hizi, ambapo tukiamua kutoa
mgawo tuliopanga tangu mwanzo wa kila kaya moja kupewa mifuko mitano ya
saruji na mabati 20 tukitaka kufanikisha hili ili waathirika waweze
kufikiwa wote tunahitaji shilingi bilioni tisa za haraka,” alieleza
Kijuu.
Alisema takwimu hizo ni za makazi ya wananchi tu ambao majengo ya
taasisi kama vile shule, makanisa, misikiti, vituo vya polisi, zahanati
na magereza havijaunganishwa humo, akibainisha kuwa wataalamu wamesema
shule moja kama ile ya Ihungo kuirudisha katika hali yake ya kawaida
zinahitajika Sh bilioni 4.5.
Alisema mpaka sasa misaada inaendelea kupokewa, na hadi kufikia
Septemba 18, vifaa mbalimbali vimepokewa na Kamati ya Maafa ya Mkoa
vyenye thamani ya Sh bilioni tano huku zaidi ya Sh milioni 663
zimeishaingizwa katika akauti ya maafa.
Aidha, alisema pia harambee iliyofanyika wiki iliyopita kwa kuongozwa
na mkuu wa mkoa fedha taslimu Sh milioni saba zilipatikana na ahadi
ikiwa Sh milioni 700.
Katika hatua nyingine, Balozi wa Kenya nchini, Chirau Ali Mwakwere
amekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali ikwemo mabati 4,000, magodoro100
na mablanketi 400 kwa niaba ya Rais Uhuru Kenyatta, na kueleza kuwa
wananchi wao na serikali yao wameguswa sana na tukio hilo ndiyo maana
wakajitoa kwa hicho kidogo ili wasaidie.
“Tunakumbuka kauli ya Mwalimu Julius Nyerere aliyotoa kuwa binadamu
wote ni ndugu na Afrika ni moja, kwa hiyo sisi ni ndugu inabidi
tusaidiane kwa shida na raha,” alisema Balozi Mwakwere na kuipongeza
Serikali ya Tanzania kuboresha miundombinu ya barabara kwani wamesafiri
kwa njia ya barabara kutoka mwanzo wa safari yao mpaka Bukoba bila
usumbufu na kuifananisha barabara hizo na za Afrika usoni.
Wakati huo huo, maofisa elimu wa shule za sekondari na msingi
zilizopo mkoani Kagera wamepewa siku tatu kukamilisha taarifa sahihi za
majengo yaliyobomoka na idadi ya wanafunzi walioathiriwa na tetemeko
huku wakitakiwa kuwa makini katika utoaji wa taarifa za tukio hilo.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa
Joyce Ndalichako alisema hayo wakati akitembelea shule zilizoathiriwa na
tetemkeko na kusababisha majengo kuanguka na nyufa kubwa kutokea katika
Wilaya ya Missenyi na Manispaa ya Bukoba.
Shule hizo ni sekondari ya Nkenge, shule ya bweni Bwabuki Nyanshenye,
shule za msingi zilizopo wilayani Missenyi pamoja na shule za sekondari
za wavulana Ihungo na Nyakato na Shule ya Msingi Mugeza Mseto ambayo ni
shule ya wanafunzi maalumu wenye ulemavu mbalimbali zilizopo Manispaa
ya Bukoba.
Profesa Ndalichako alisema ikiwa ni siku nane tangu kutokea kwa ajali
hiyo, maofisa elimu wangekuwa na taarifa sahihi za majengo
yaliyoharibika zaidi na yale yaliyo na nyufa.
“Taarifa hizi zinakuwa kama za kubahatisha, umakini unatakiwa kwa
hili, ndani ya siku tatu lazima kupata taarifa ambazo zimechambuliwa
vizuri na zenye kuonesha wapi kuna tatizo,” alieleza na kuongeza kuwa
katika shule hizo zilizoharibika wanafunzi watatafutiwa sehemu nyingine
ya kuendelea na masomo yao wakati shule walizokuwa wakisomea zikijengwa
na shule nyingine kufanyiwa ukarabati kwa ubora zaidi.
chanzo;habarileo.
Comments