WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa
Joyce Ndalichako, amewataka vijana waliopo masomoni na wahitimu nchini,
kuhakikisha wanajifunza zaidi mbinu za kujiajiri na si kusubiri
kuajiriwa.
Aidha Waziri huyo, ametoa changamoto kwa taasisi za elimu ikiwemo
vyuo vikuu kuzalisha wahitimu wenye taaluma na mikakati itakayowezesha
kujiajiri na si wahitimu wanaotafuta ajira.
Aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika hotuba iliyosomwa kwa niaba
yake na Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi Nicholaus Burreta wakati wa ufunguzi wa Kongamano la
Vijana, linalohusu mikakati ya kumaliza tatizo la ajira na rushwa.
“Ni kweli tatizo la rushwa ni kubwa si hapa nchini bali Afrika nzima
kwa ujumla. Afrika ina watu takribani bilioni moja lakini kati yao
milioni 50 hawana ajira. Nawapongeza vijana kwa kuliona hili na kuamua
kulivalia njuga ili kulipatia ufumbuzi,” alisema.
Alisema wakati dawa ya ukosefu wa ajira ikiendelea kutafutwa duniani
kote, ni wakati sasa kwa vijana wa kitanzania kuwa na mabadiliko ya
kifikra na pindi wanapohitimu wajitahidi kuwa na elimu ya ziada
itayowawezesha kujiajiri na si kusubiri ajira.
“Nasema tuachane na wasomi wanaosubiri ajira, hata taasisi za elimu
ikiwemo vyuo vikuu tutengeneze vijana wenye mitazamo chanya ya kujiajiri
wenyewe. Hili si tu litawakwamua kiuchumi lakini pia litaongezea na
kulijenga taifa kiuchumi,” alisema.
Alisema hali ya kuendelea kutoa elimu inayowafanya vijana wategemee
zaidi kuajiriwa ndio inayochangia kuwepo na tatizo kubwa la ukosefu wa
ajira kwa vijana wengi ambao matokeo yake huishia vijiweni.
Akizungumzia tatizo la rushwa, alisema tatizo hilo pamoja na
kuendelea kutafuna nchi pia limekuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji
wa utawala bora katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.
Alisema tumaini la nchi yoyote ile ni vijana hivyo ni vyema taasisi
husika ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
ikaanza kushirikisha kwa ukaribu zaidi vijana katika kudhibiti vitendo
vya rushwa.
Kwa upande wake, Burreta alisema anaamini kuwa njia pekee
itakayosaidia katika kupambana na tatizo la rushwa si kuwapatia maslahi
bora watumishi wa umma au wafanyakazi tu bali ni kuwabadili mtazamo wao
ili waichukie kabisa rushwa.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Vijana (AYLTS), Nesia Malunje, alisema
mkutano huo umewakutanisha vijana kutoka nchi 14 za Afrika baadhi yake
ni Rwanda, Uganda na Sudan Kusini kwa lengo la kujadili na kutafuta
ufumbuzi dhidi ya matatizo ya ukosefu wa ajira na rushwa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkaazi Shirika la Umoja wa Mataifa, Stella
Vuzzo, alisema uamuzi huo wa vijana kukutana na kuzungumzia matatizo ya
ajira na rushwa ni muhimu kwani unaendana na malengo 17 ya Maendeleo
Endelevu (SDGs) yanayotekelezwa na nchi takribani 193 wanachama wa UN
ikiwemo Tanzania.
Awali, akiwasilisha matokeo ya utafiti kuhusu hali ya ajira kwa
vijana nchini Tanzania, Meneja Utafiti kutoka AYLTS, Elizabeth Nkanda,
alisema matokeo ya utafiti huo uliowahoji vijana takribani 3,000 nchi
nzima yanaonesha kuwa asilimia 78 wanalalamikia tatizo la ukosefu wa
ajira na rushwa.
chanzo;habarileo.
Comments