MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameamuru posho walizokuwa
wakilipwa madiwani wa Jiji la Arusha, zinazofikia zaidi ya mamilioni ya
fedha kwa ajili ya vikao, nauli, mafuta na vocha za simu, kubadilishwa
matumizi na kulipa madeni ya walimu wanaodai zaidi ya Sh milioni 154.
Amesema kila mwalimu anastahili kusimamia mitihani na kupata posho na
si baadhi ya walimu kusimamia mitihani hiyo mara kwa mara kama vile
hakuna wengine.
Uamuzi huo wa Gambo aliutoa jana wakati alipozungumza na walimu wa
shule za msingi na sekondari, walimu wakuu, waratibu wa elimu kata
pamoja na wakuu wa vitengo mbalimbali za utumishi wa umma akiwemo Mkuu
wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro na Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la
Arusha, Athumani Kihamia.
Gambo amesema fedha hizo zilizobadilishwa matumizi yake, zinatoka
kwenye posho walizokuwa wakilipana madiwani hao kwenye sikukuu, ambazo
Mkurugenzi wa Jiji aliyekuwepo kabla ya wa sasa na Meya walikuwa
wakilipana Sh milioni moja kila sikukuu, Sh milioni 61.2 za simu, nauli
Sh milioni 28 na gharama za mafuta ambazo wamekuwa walipwa madiwani hao
kulingana na umbali, ikiwemo posho ya dereva anayetoka nje ya mkoa Sh
100,000 kwa siku na kulipwa kadri ya siku atakazokaa.
Amesema fedha hizo ni nyingi na hivi sasa zimesitishwa matumizi yake,
badala yake madiwani hao watalipwa Sh 10,000 kama nauli kwa ajili ya
kuja kwenye vikao vya Baraza la Madiwani na posho zao za vikao, ambazo
pia zimepunguzwa.
Amesema haiwezekani walimu wadai zaidi ya Sh milioni 154 ambazo jiji
linaweza kuwalipa kulingana na vyanzo vya mapato vya ndani, badala yake
madiwani ndio wanufaike na fedha hizo huku kila sikukuu wakijilipa posho
kubwa na watumishi wengine wakishindwa kutatuliwa kero zao na
kuzungushwa tu.
“Haiwezekani walimu wawe wanaidai serikali zaidi ya shilingi milioni
154 wakashindwa kulipwa huku wakifanya kazi kwenye mazingira magumu
halafu wengine wanakula raha…sasa nasema walimu walipwe fedha hizi ndani
ya wiki mbili na fedha hizi walikuwa wakilipwa madiwani sasa nasema
walimu walipwe madeni yao ikiwemo malimbikizo ya nauli na fedha za
kupandishwa madaraja,” amesema Gambo.
Amewaagiza mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa jiji kuhakikisha
wanakwenda kuangalia shule za sekondari na msingi na kuzikagua ili
kujionea hali halisi sambamba na kuwaagiza wakuu wa shule mbalimbali za
msingi na sekondari kuanisha ni nyumba ngapi zinahitajika kwaajili ya
ujenzi wa nyumba za walimu.
Amewataka wakuu wa shule za sekondari na msingi kutoa nafasi kwa
walimu wengine kusimamia mitihani na fursa nyingine zinazojitokeza
badala ya kufanya upendeleo kwa baadhi ya walimu ikiwemo kupandishwa
madaraja walimu wasiostahili kunakotokana na kujipendekeza kwa wakuu wa
shule au kutoa rushwa ya ngono kupata fursa hizo.
chanzo;habarileo.
Comments