MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemtaka Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) anayekabiliwa na mashitaka ya
uchochezi, afike mahakamani leo kujieleza kwa nini asifutiwe dhamana.
Lissu anatakiwa ajieleze kwa sababu yeye a mdhamini wake hawakufika
mahakamani jana wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya kutoa uamuzi wa
pingamizi la upande wa utetezi.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alitoa amri hiyo jana baada ya Wakili
wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi kuomba Mahakama itoe hati ya
kumkamata Lissu kwa sababu ya kutokufika mahakamani.
Awali akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba alitupilia mbali pingamizi la
upande wa utetezi na kuruhusu upande wa Jamhuri kuleta upya mashitaka
mawili ya uchochezi, ambayo hapo awali yalifutwa kwa kuwa hayakuwa na
kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Alisema awali mashitaka hayo yaliondolewa kwa sababu hayakuwa na
kibali lakini sasa ameyakubali kwa sababu yamewasilishwa pamoja na
kibali cha DPP, pia upande wa Jamhuri ulikuwa na haki ya kurekebisha
mapungufu na kuyaleta tena mashitaka hayo mahakamani.
Hata hivyo, baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Wakili wa Utetezi,
Peter Kibatala alidai hawajaridhika, hivyo wanatarajiwa kukata rufaa
kuupinga kwa sababu mashitaka hayo yalipofutwa yalikuwa yamekufa.
Aidha, aliiomba Mahakama kutoyasoma mashitaka hayo hadi rufaa yao
itakaposikilizwa katika Mahakama Kuu na kutolewa uamuzi. Wakili wa
Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa upelelezi wa kesi
hiyo umekwishakamilika.
Hivi karibuni upande wa utetezi uliwasilisha pingamizi hilo, baada
Wakili Kishenyi kuomba kuwasomea washtakiwa hati iliyofanyiwa
marekebisho kwa kuongeza mashitaka mawili, ambayo awali yalishafutwa.
Katika pingamizi hilo, wakili alipinga washtakiwa hao kusomewa upya
mashitaka hayo kwa kuwa mashtaka mapya, hayatofautiani na yale
yaliyofutwa mahakamani hapo Juni 28, mwaka huu.
Akijibu hoja hizo, Kishenyi alidai shtaka la kwanza na la tano ni
kama hayakuwepo mahakamani na kwamba kuondolewa kwake sheria haikatazi
kuyarudisha tena.
Mbali na Lissu washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa
gazeti la Mawio, Simon Mkina, mwandishi wa gazeti hilo, Jabir Idrisa na
Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Wanadaiwa kati ya Januari 12 na 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa
lengo la kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar, Jabir, Mkina na Lissu,
kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa
cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Katika mashtaka yanayomkabili Mehboob, anadaiwa, Januari 13 katika
jengo la Jamana, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa
na taarifa za uchochezi, pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha
hati ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
chanzo;habarileo.
Comments