MKUTANO wa Nne wa Bunge la 11 unatarajiwa kuanza leo mjini hapa, huku
miswada sita ukiwemo wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari ukitarajiwa
kuchukua nafasi kubwa.
Katika mkutano huo, wabunge wa kambi ya upinzani ambao walisusia siku kadhaa za mkutano uliopita, wamesema kwamba watahudhuria.
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alithibitisha jana kwamba wabunge wa upinzani wataingia bungeni.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya
Bunge kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, jumla ya maswali 110
yanatarajiwa kuulizwa na wabunge na kujibiwa na Serikali.
Aidha, Waziri Mkuu anatarajiwa kuulizwa maswali 16 ya papo kwa hapo.
Taarifa hiyo ilisema miswada sita ya sheria iliyosomwa kwa mara ya
kwanza katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na baadaye kupelekwa katika
kamati husika ili ifanyiwe kazi, itaendelea kushughulikiwa katika hatua
zinazofuata ikiwa ni pamoja na kusomwa kwa mara ya pili, kamati ya Bunge
zima na kusomwa kwa mara ya tatu.
Miswada hiyo ni pamoja na ule wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari ya
mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Utathmini na Usajili wa Wathamini wa
mwaka 2016, Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serika wa mwaka 2016.
Pia utakuwepo Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia
wa mwaka 2016, Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo wa
mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi ya mwaka
2016.
Kufikia jana, mji wa Dodoma ulikuwa umefurika wageni balimbali
wakiwemo wabunge na maofisa wa serikali wanaohamia tayari kuanza
kuendesha shughuli zao katika makao makuu mapya ya Serikali, mjini hapa.
chanzo;habarileo.
Comments