RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameongoza mamia ya wananchi
katika maziko ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Pili na Makamu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Aboud Jumbe Mwinyi
yaliyofanyika nyumbani kwake Migombani Unguja.
Mwili wa marehemu uliwasili mapema asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa
Abeid Amaan Karume, na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo ulifikishwa nyumbani kwake kabla ya
kupelekwa katika Msikiti wa Mwembeshauri mjini Unguja kwa ibada.
Ibada ya kumswalia marehemu ilifanyika katika msikiti huo, ambao
ujenzi wake kwa kiasi kikubwa mchango wake umetokana na Jumbe mwaka
1982. Sala ya maiti iliongozwa na Mufti wa Zanzibar, Shehe Saleh Kabi
ambaye alimtaja Jumbe kuwa kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika
kuimarisha amani na utulivu kwa kujenga uvumilivu wa kisiasa.
“Waislamu tunapaswa kuiga mfano wa Alhaji Jumbe katika kuimarisha
umoja na kujenga tabia ya kuvumiliana na kuomba msamaha kwa pale
anapowakosea watu,” alisema.
Safari ya mwisho ya Mzee Jumbe, ilianza nyumbani kwake Migombani
ambapo alizikwa kwa heshima zote za Serikali zote mbili, ambazo
alizitumikia katika kipindi kirefu cha uhai wake. Dk Shein aliongoza
kuweka udongo katika kaburi la marehemu, ambalo lipo karibu na makaburi
mengine manne ya watoto wake, waliozikwa jirani na eneo hilo.
Alifuatiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadaye Rais mstaafu wa
Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.
Wengine waliopata fursa ya kuweka udongo katika kaburi la marehemu ni
Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali
Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Viongozi wengine ni Jaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman
Makungu na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid.
Walikuwepo pia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine
Mahiga, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na
Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka.
Dua ya kumuombea marehemu ilisomwa na Shehe Mohd Kassim kutoka katika
Ofisi ya Wakfu na Mali ya Amana. Msemaji wa familia, Mustafa Aboud
Jumbe alizishukuru serikali zote mbili kwa kumhudumia katika kipindi
chote, ikiwemo matibabu ya nje ya nchi na ya ndani.
“Tunazishukuru Serikali zote mbili kwa kumhudumia mzee katika kipindi
chote cha ugonjwa wake kwa kumsafirisha nje ya nchi na kupata matibabu
ya ndani,” alisema Jumbe.
Baadhi ya viongozi walimuelezea Mzee Jumbe kuwa ni nguzo imara ya
Chama Cha Mapinduzi, kwa kuunda chama ambacho nguvu zake zimekuwa imara
hadi leo kwa kushinda katika chaguzi mbalimbali katika mfumo wa vyama
vingi.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mohamed Ramia alimtaja Jumbe kama kiongozi
aliyekuwa akiwaamini vijana kushika nafasi za uongozi, ikiwemo yeye
kumpa nafasi hiyo nyeti.
Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Dk Salim
Ahmed Salim alimtaja Mzee Jumbe kuwa ni kiongozi hodari, ambaye
alimsaidia wakati aliposhika madaraka na nyadhifa mbalimbali za uongozi.
Dk Salim alisema alianza kukutana na Jumbe wakati akiwa mwalimu wake
katika Shule ya Sekondari Lumumba katika miaka ya 1958.
Aboud Talib Aboud ni mwanafunzi wa Mzee Aboud Jumbe, ambaye alipata
kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi yake na kujiuzulu na anamtaja Jumbe
kuwa kiongozi na mwanasiasa aliyepevuka akiwa na muono wa mbali.
Miongoni mwa wanafunzi wake wa darasani ni Maalim Seif Sharif Hamad,
ambaye alimteua kuwa msaidizi wake katika Ofisi ya Rais hadi kuwa Waziri
wa Elimu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miaka ya 1983.
Waziri wa Ujenzi, Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar, Balozi Ali Karume anamtaja Mzee Jumbe kuwa ni sawa na baba
yake mzazi, ambaye alichukuwa nafasi kubwa ya kumfariji baada ya baba
yake aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kuuawa.
Ramadhan Abdalla Shaaban ni Waziri aliyefanya kazi na Alhaji Jumbe
akiwa Waziri wa Biashara na Viwanda katika miaka ya 1983, ambaye
anamtaja kuwa kiongozi aliyefanya kazi naye vizuri kwa ufanisi mkubwa.
Aliutaja mchango wa Jumbe kuwa ni pamoja na kuanzisha Baraza la
Wawakilishi katika mwaka 1979 pamoja na Katiba ya mwaka 1984, kwa
kutenganisha mihimili miwili ya dola kwa ajili ya kufanya kazi zake kwa
ufanisi mkubwa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Ali Abdallah Uchupa alisema
alifanya kazi karibu na hayati Jumbe wakati akiwa katika chama hicho.
chanzo;habarileo.
Comments