Pangani wamshukuru Magufuli kuwapatia kivuko.

WAKAZI wa Wilaya ya Pangani mkoani Tanga wamemshukuru Rais John Magufuli kwa kutimiza haraka ahadi yake ya kuwapatia kivuko kipya cha Mv Tanga, kinachounganisha mji huo wa kihistoria na maeneo mengine yaliyoko ng’ambo ya Mto Pangani.

Walibainisha hayo walipozungumza jana kwa nyakati tofauti katika mahojiano wakati kivuko hicho kilichojengwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport Limited ya Dar es Salaam, kilipowasili mjini humo na kupokewa na wananchi pamoja na baadhi ya viongozi wa Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme nchini (Temesa).

Ali Mtoto mkazi wa Bweni alisema ana furaha kubwa kwa kivuko hicho kuwasili kwa sababu kitawapunguzia adha na usumbufu walioupata kwa muda mrefu walipolazimika kutegemea kivuko kimoja cha Mv Pangani II.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Le-Kujan Manase alisema baada ya kukipokea kutoka kwa mkandarasi na kufanyiwa majaribio wameridhika kwamba kipo vizuri tayari kwa ajili ya kuhudumia wananchi.

Manase alisema katika ujenzi wa kivuko hicho cha Mv Tanga, serikali imegharamia dola za Marekani 1, 869,000 hadi kukamilisha ujenzi huo. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi wa kivuko hicho, Salehe Songoro aliishukuru serikali kwa kuiamini kampuni hiyo hadi kuipatia kazi hiyo.

chanzo;habarileo.

Comments