MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Marcelin Ndimbwa
ametekeleza ahadi yake na kuunga mkono maagizo ya serikali ya kuondoa
umaskini kwa vijana kwa kushawishi wahitimu 35 wa vyuo vikuu kujiunga na
mradi wa kilimo cha mpunga wilayani humo.
Kupitia mpango wake huo, mkurugenzi huyo amewawezesha wasomi hao
kuungana na kupewa ekari 45 za kulima zao hilo, lakini akisema
watawezeshwa zaidi kwa kupewa mbegu za kisasa bure ambazo zitawawezesha
kupata mavuno baada ya siku 85.
Mkurugenzi huyo kwa ushirikiano mkubwa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi,
Matiku Majura wamekuwa wakibuni mikakati ya kuwakomboa Watanzania
kutokana na agizo la Rais John Magufuli la kuwataka viongozi kusimamia
maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika
Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, ambaye ni Ofisa Kilimo, Mhandisi
Maimuna Makutika, wasomi hao watanufaika na kilimo hicho kwa kuzalisha
magunia kati ya 40 hadi 50.
Akizungumzia gharama za kilimo hicho, Mhandisi Makutika alisema
kilimo hicho ni nafuu kutokana na mkulima kutumia pungufu ya Sh 600,000
hadi mavuno kwa ekari moja na baadaye kupata faida kwa kuuza gunia moja
kati ya Sh 80,000 na Sh 120,000.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Ndimbwa alisema kupitia uwekezaji huo,
vijana hao watakuwa wamepata ajira ya kudumu lakini pia watakuwa
wamejikwamua kiuchumi kama watafanya bidii na kuyatunza mashamba hayo
inavyostahili.
Alisema tayari vikundi vya vijana wilayani hapo vimehamasika baada ya
kuona mwitikio wa wasomi kuwekeza kwenye kilimo na kwamba mpaka sasa
vijana wenyeji walioitikia ni zaidi ya 150, vikundi 30 na ekari zaidi ya
200 zimeshalimwa.
chanzo;habarileo
Comments