
Hali hiyo imedhihirisha namna chuki za kisiasa
visiwani humo zilivyotamalaki ambapo Maalim Seif na Dk. Shein ndio mara
ya kwanza kukutana uso kwa uso baada ya Uchaguzi Mkuu wa marudio
uliofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu visiwani Zanzibar.
Dk. Shein ndiye aliyekuwa akiongoza mazishi ya Alhaj Jumbe ambaye
alikuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)
aliyefariki Jumapili wiki iliyopita.
Kwenye msiba huo, baada ya Dk. Shein kusalimiana na wageni wengine
kwa kuwapa mkono, alipofika kwa Maalim Seif, Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF), aligoma kupokea mkono wake.
Baada ya Maalim Seif kutopokea mkono wake, Dk. Shein aliunyoosha tena
kwa matumaini kwamba kiongozi huyo wa CUF angeupokea, hata hivyo Maalim
Seif aligoma.
Kutokana na mgomo huo, Dk. Shein alilazimika kumruka na kuendelea
kusalimiana kwa kupeana mikono na viongozi wengine waliohudhuria maziko
hayo.
Hatua hiyo imepokewa kwa hofu na baadhi ya waombolezaji waliokuwepo kwenye eneo hilo na walioshuhudia tukio hilo.
Hali hiyo inatafsirika kuwa ni kilele cha chuki za kisiasa
zilizochochewa na Tume ya Uchaguzi visiwani Zanzibar (ZEC) chini ya
mwenyekiti wake Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu
kinyume na Katiba ya visiwa hivyo.
Kabla ya tukio hilo, visiwani Zanzibar kumeripotiwa kuwepo kwa
ubaguzi wa kisiasa katika mambo mbalimbali ikiwemo huduma za kijamii
ambapo wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanalalamika kutengwa na
wale wa CUF.
Miongoni mwa maeneo yanayolalamikiwa kuwepo kwa ubaguzi huo ni katika
uuzaji wa bidhaa dukani, usafiri wa daladala pamoja na vikao vya pamoja
vya kijamii.
Mara kadhaa Jeshi la Polisi limekuwa likimwita Maalim Seif kwa
mahojiano kutokana na matukio mbalimbali yanayoendelea visiwani humo.
Hata hivyo Jeshi la Polisi visiwani humo wamekuwa waoga kueleza kiini
cha mahojiano hayo ambapo viongozi wa CUF wamekuwa wakieleza kuwa ni
kutokana na tuhuma za uchochezi.
Serikali ya Dk. Shein inayumba kutokana na baadhi ya Wazanzibari
kuipa mgongo kwa tuhuma kwamba, urais aliotunukiwa na NEC hauna ridhaa
ya wananchi wa visiwa hivyO.
CHANZO; mwanahalisionline.
Comments