DC:Viongozi waliotoroka na trekta la kijiji wasakwe.

MKUU wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, Majura Kasika, ameliagiza Jeshi la Polisi kusaka na kumchukulia hatua za kisheria diwani wa zamani wa Kata ya Ngoherenga, Pius Mwalase na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Novatus Mvogo kwa tuhuma za kutoweka na trekta la kijiji pamoja na maelfu ya michango ya fedha.

Agizo hilo la kusakwa na kukamatwa kwa watu hao ni baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo kupokea malalamiko ya wananchi wa kata hiyo kuwa tangu trekta hilo linunuliwe kwa mkopo wa Sh mil 50 kutoka Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA –JKT) mwaka 2012/2013 halipo kijijini hapo.

Wananchi hao walidai kuwa waliokuwa viongozi wa Kata ya Ngoherenga kwa kushirikiana na kijiji hicho hawakuwahi kusoma mapato na matumizi ya mradi wa trekta hadi sasa na kwamba trekta hilo halijilikani lilipo.

Walidai kwa nyakati tofauti kuwa viongozi hao wa zamani akiwemo aliyekuwa diwani wa kata pamoja na mtendaji wa kijiji walitoroka na mali mbalimbali za kijiji ikiwemo fedha za michango Sh mil 1.1.

Fedha hizo na matumizi yake katika mabano ni Sh 442,000 (mchango wa umeme ), Sh 110,000 (michango ya matofali) na nyingine zikiwa ni fedha za kijiji Sh 585,000 pamoja na trekta lililonunuliwa kwa njia ya mkopo kutoka SUMA-JKT.

Kutokana na malalamiko hayo, Mkuu wa wilaya hiyo alitoa maagizo ya serikali ya wilaya kwa kuagiza vyombo vya dola kuwatafuta mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Katika hatua nyingine, aliwahakikishia wananchi wa Malinyi kuwa hatua mbalimbali zimechukuliwa kwa kuanzisha doria katika barabara ya Lupiro-Malinyi ili kukabiliana na majambazi wanaofanya vitendo vya utekaji wa magari ya abiria na mizigo.

chanzo;habarileo.

Comments