Beit al-Ajaib, lulu ya Zanzibar.

VISIWA vya Zanzibar ni maarufu Afrika ya Mashariki na duniani kote kutokana na kuwa historia ya pekee.

Mbali na historia yake, Zanzibar imekuwa ni eneo linalowavutia watu wengi kutokana na kuwa na mandhari nzuri zikiwemo, fukwe, mzunguko wa bahari, Bustani ya Forodhani, wanyama adimu kama vile kima na punju, hoteli za kitalii na Mji Mkongwe ambao ni rasilimali kubwa katika sekta ya utalii.

Kadhalika pamoja na nchi kupata fedha za kigeni, wananchi wengi wamekuwa wakifaidika na sekta hiyo ya utalii kwa kujipatia ajira na hivyo kuwa sababu ya kupata pesa za kujikimu kimaisha ambapo vijana wengi hupata kazi mbalimbali ikiwemo ya kuongoza watalii, hasa katika eneo la Mji Mkongwe.

Moja ya eneo la kuvutia ndani ya Mji Mkongwe na jengo la Beit -Al Ajaib, neno lenye asili ya Kiarabu likimaanisha “nyumba ya maajabu”. Jengo hili refu na pana kuliko yote katika eneo la Mji Mkongwe hutembelewa na watalii wengi ili, mbali ya kufurahia mandhari ya jengo hilo, hupata pia kujua historia yake.

Mji Mkongwe una sifa ya kuitwa mji wa kale hasa kutokana na mvuto na mandhari ya majengo yake ya kale ambayo mbali na Beit -Al Ajaib ambayo tunaweza kusema ndilo jengo ‘baba yao’, lakini pia kuna majengo mengi ya kihistoria kama nyumba ya hukum (Beit el Hukum), Beit el Sahel, Bandari ya Waarabu (Arab Fort), Nyumba ya Amani (museum) na mengine mengi ambayo yanavutia kutazama kutokana na ujenzi wake wa kizamani na kuwa na kumbukumbu zinazoelekeza hata leo.

Kutokana na Zanzibar kutawaliwa na Sultani wa Oman mnamo mwaka 1828 -1858, Seyyid Said bin Sultan ambaye alifungua kurasa ya falme hizo, hivyo kujenga ukurasa wa historia ambayo imekuwa pia kivutio cha wengi leo. Mji Mkongwe umeendelea kujizolea umaarufu na hasa ulipoingia kwenye miji yenye sifa za urithi wa dunia. Watalii mbalimbali wanaokuja kutembelea Zanzibar na maeneo yake, hawakosi kuitembelea nyumba hiyo ya maajabu na yenye historia ya pekee Afrika ya Mashariki na duniani kote.

Beit el Ajaib ilijengwa na Sultan Said Barghash aliyetawala Zanzibar kati ya 1870-1888 na mnamo mwaka 1880 ikawa kasri kwa ajili ya sherehe mbalimbali za kiserikali na kupokelea wageni. Na liliitwa jumba la maajabu kutokana na sababu nyingi, kubwa ni kuwa jengo la kwanza kupata umeme visiwani humo. Ilijengwa kwa mfano wa nyumba za Oman ambazo zilikuwa za kisasa sana kwa wakati huo. Ina veranda za nje zilizojengwa na baadaye kuinuliwa kwa nguzo za chuma.

Ina milango ya kazi 13 yenye ilham ya Kihindi ikiwa na kizingiti cha juu cha umbo la nusu duara na maumbo ya wanyama mbalimbali pamoja na maandishi ya Kiarabu. Mfalme huyo wa tatu kutawala Zanzibar, yaani Seyyid Barghash, alipoingia madarakani mnamo 1870 aliifanya Zanzibar kuwa makao makuu ya serikali ya Oman na hivyo kujulikana kama sehemu ya nchi hiyo, hatua ambayo imekuwa pia ikizidisha historia ya kuvutia ya Zanzibar.

Jengo la Beit el Ajaib ambalo linasaidia kutambulisha utamaduni wa Mzanzibari, kwa sasa lina umri wa miaka 193, yaani takribani karne mbili lakini bado liko imara. Lina vyumba virefu visivyopungua mita 40 na kuendelea, kuta zake zimejengwa kwa mchanganyiko wa udongo, chokaa na mawe na kama ilivyoelezwa hapo juu zinazoonekana ni madhubuti zaidi kuliko kuta za majengo ya matofali na mchanga ya zama hizi. Hali hiyo inaonesha kwamba jengo linaweza kuishia karne nyingine ijayo likiwa madhubuti.

Ingawa jengo hilo ambalo pia lilijulikana zamani kama Nyumba ya Barghash, lina ghorofa mbili tu, lakini kwa urefu, kama lingejengwa zama hizi kutokana na urefu wake, pengine lingekuwa na ghorofa kati ya 5 na 6. Hata hivyo, kutokana na uchakavu wa majengo hayo ya zamani, Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (Unesco) limekuwa likihimiza kuyahifadhi kwa kurudisha mbinu za asili za ujenzi wa majengo hayo katika kuboresha mandhari yake lakini bila kuathiri uasili wake.

Wafalme waliotawala Zanzibar na kujenga historia na mandhari ya Mji Mkongwe tunayoshudia leo ni pamoja na Seyyid Said bin Sultan (1828-1856), Sultan Majid Bin Said (1856-1870), Sultan Barghash bin Said (1870 -1888), Sultan Khalifa bin Said (1890-1892), Sultan Ali bin Said (1892-1894) na Sultan Hemed bin Thuwein (1894-1896). Wengine ni Sultan Hamoud bin Mohamed (1896-1902), Sultan Ali bin Hamoud (1902-1911), Sultan Khalifa bin Hroub (1911-1960), Sultan Abdallah bin Khalifa na Sultan Jamshid bin Abdullah 1963-1964.

chanzo;habarileo.

Comments