KAMANDA wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro
amewaagiza askari kuhakikisha wanampata akiwa hai au amekufa mhalifu
aliyetekeleza mauaji ya kinyama ya askari wa kikosi cha usalama
barabarani, Sajini Mensah Ponda Dishe.
Aidha, amesema hata kama mtu aliyefanya unyama huo yuko ndani ya
familia, jeshi hilo litahakikisha linamshughulikia ipasavyo ili haki
ipatikane.
Aliyasema hayo jana wakati akiongoza mamia ya askari na wananchi
waliojitokeza kuuaga mwili wa askari huyo katika viwanja vya nyumba za
polisi Kunduchi. “…Nimewaambia askari walio chini yangu wafanye kila
liwezekanalo ili mhalifu aliyehusika kufanya tukio hili la kinyama
akamatwe akiwa mzima au akamatwe akiwa amekufa ili haki itendeke,”
alisema Kamanda Sirro.
Alisema hata kama mhalifu huyo atabainika kuwa yuko ndani ya familia
ya askari huyo, Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua za kisheria
ili kuhakikisha haki imepatikana.
Kamanda Sirro alisema, alipopata taarifa za askari huyo kupigwa
risasi alikwenda hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini aliambiwa
kuwa amepelekwa Hospitali ya Mwananyamala ambapo alipofika aliambiwa
kuwa ameshapoteza maisha kwa kuwa alipigwa risasi kwa karibu sana.
Alisisitiza askari wote kuhakikisha wanatenda haki, wanakataa rushwa
ili hata siku ya mwisho wakati wa hukumu ya Mwenyezi Mungu waweze kwenda
sehemu salama.
chanzo;habarileo.
Comments