WIZARA ya Nishati imesema imejipanga kuhakikisha Dodoma inakuwa na
umeme wa uhakika wakati nchi itakapohamia rasmi ili kukidhi mahitaji
kutokana na ongezeko la watu litakalotokea mkoani humo.
“Sasa tunajipanga kuhakikisha kunakuwa na umeme wa kutosha kuondokana
na habari za kukatika katika kwa umeme kwani uwepo wa makao makuu
utaongeza matumizi ya umeme kutokana na idadi ya watu kuongezeka na hata
ujenzi utaongezeka.”
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema hayo
jana mjini hapa wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi
kujenga njia ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa kilovoti 400
ujulikanao kama “Backbone Transmission Investment Project” ambao
unajengwa kutoka Iringa mpaka Shinyanga kupitia Dodoma na Singida.
Alisema mahitaji ya umeme katika mkoa wa Dodoma ni megawati 25.2 na
sasa wanajipanga kuhakikisha makao makuu hayo ya nchi yanakuwa na
uhakika wa umeme siku zijazo.
Alisema umeme wa megawati 60 utatosha Dodoma.
“Kesho (Leo) kutakuwa na kikao kati ya Wizara ya Nishati, Mamlaka ya
Ustawishaji makao makuu (CDA) na Shirika la Umeme (Tanesco) kuona namna
ambayo kwa miaka ijayo umeme unakuwa wa kutosha.
Alisema kukamilika kwa miradi ya backbone kutasaidia nchi kuwa na umeme wa uhakika na hata ziada kuuzwa nje ya nchi.
“Tunataka kuingia kwenye power trade (biashara ya umeme) nchi
nyingine kama Ujerumani wanauzia umeme Ufaransa kwa nini sisi tusiweze,”
alisema Profesa Muhongo.
Alisema Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi chache Afrika zenye umeme wa msongo mkubwa kama huo.
Alisema Septemba mwaka huu, Rais John Magufuli atazindua mradi wa
ujenzi wa njia ya umeme kutoka Iringa hadi Dodoma ambao umekamilika kwa
asilimia 100.
Alisema miradi ya umeme ya kutoka Dodoma hadi Singida na Singida hadi Shinyanga itakamilika Oktoba mwaka huu.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi huo, James Khalid alisema mradi
huo umegawanywa katika makundi matatu ambapo nguzo kubwa zenye kubeba
nyaya za kupitisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 imejengwa kutokea Iringa
hadi Dodoma kwa gharama ya dola za Marekani milioni 150, fedha kutoka
benki ya dunia na mradi huo umekamilika kwa asilimia 100.
Sehemu ya pili ni Dodoma hadi Singida inajengwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni 169.
Alisema fedha ni kutoka Japan na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
na sehemu ya tatu ni Singida hadi Shinyanga ambayo inajengwa kwa gharama
ya dola za kimarekani milioni 134.7 kutoka European Investment Bank
ambapo miradi hiyo miwili itakamilika Oktoba mwaka huu na kukabidhiwa
kwa serikali.
Pia serikali ya Tanzania ilitoa fedha za kulipa fidia Sh bilioni 23.
Mradi huo unafadhiliwa kwa pamoja kati ya serikali ya Tanzania, Benki ya
Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Exim ya Korea na
Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ambapo wawakilishi wake walikuwa
kwenye ziara hiyo ya Waziri.
chanzo;habarileo.
Comments