MAWAKILI
wa kujitegema zaidi ya 100 mkoani Arusha, jana waliandamana kwenda kwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, kulaani kile
walichokiita ukandamizwaji wa sheria za nchi na kazi ya uwakili
unaofanywa na polisi.
Wanasheria
hao wanalaani kitendo cha wakili mwenzao, Shilinde Ngalula, kukamatwa,
kufungwa pingu na kufunguliwa mashtaka akiwa kazini Loliondo wilayani
Ngorogoro.
Mawakili
hao walitembea zaidi ya hatua 400 kabla ya kuzingirwa na polisi ambao
waliwataka kuunda kamati ya watu wachache kwenda kuzungumza na Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo.
Uamuzi
wa kufanya maandamano hayo, ulipitishwa jana mjini hapa baada ya
mawakili hao kufanya kikao cha pamoja viwanja vya Mahakama ya Hakimu
Mkazi Arusha.
Awali,
mawakili hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika
(TLS), Wakili Modest Akida, pia walikubaliana kutoendelea na kesi za
wateja wao waliokuwa mahakamani.
Akizungumzia
maandamano hayo, Akida alisema yalilenga kupinga kitendo cha Jeshi la
Polisi wilayani Ngorongoro, kumkamata na kumfungulia mashitaka Wakili
Ngalula.
Wakiwa
tayari wameandamana umbali wa takribani hatua 400 kutoka mahakamani
hapo, vikosi vya askari polisi waliovalia kiraia na wale wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa ndani ya magari mawili, waliwazunguka na
kuwaamuru kusimama.
Mkuu
wa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Thomas Mareko, aliwataka wanasheria
hao kufuata sheria katika kudai na kuwasilisha malalamiko yao.
“Nyinyi
ni wanasheria, mpaka hapa tayari mmeshaandamana kinyume cha sheria za
nchi, nawaomba chagueni wawakilishi nitawasindikiza mnakokwenda na
wengine rudini mkaendelee na majukumu yenu,” alisema Mareko.
Baada
ya maandamano hayo kuzuiwa, mawakili hao waliwachagua wawakilishi
waliokwenda kuwasilisha malalamiko yao kwa Kamanda Mkumbo na wengine
walirudi katika viwanja vya mahakama kusubiri taarifa.
Awali, akizungumza katika viwanja hivyo, Wakili George Njooka alisema mawakili nchini wameanza kudharauliwa na vyombo vya dola.
“Hawa
watu walianza na vyombo vya habari, wakaenda kwa wanasiasa na sasa
wamekuja kwa mawakili, nawaomba tuanzie hapa twende kwa RPC atuambie
haya maelekezo tunayoambiwa yanatoka juu, yanatoka kwa nani,” alisema Wakili Njooka.
Wakili Qamara Peter aliwakumbusha mawakili wenzake kuwa haki siku zote haiombwi bali inadaiwa.
chanzo;mpekuziblog.
Comments