SERIKALI
imeanza mkakati mpya wa kuandikisha wananchi waliopo kwenye vijiji na
vitongoji kwa njia ya kielektroniki ili kupata takwimu sahihi
zitakazosaidia utoaji wa huduma bora kwa jamii.
Pia
mfumo huo utatambua watu wadanganyifu ambao wamekuwa wakidanganya
wanakotoka, ikiwemo wezi na majambazi ambao ni lazima waeleze
wanakoishi, wanakotokea, jina la mkuu wa kaya wake na namba ya
utambulisho wake.
Mfumo
huo ambao utasaidia kujua watoto waliozaliwa na watu waliokufa, taarifa
zitakazotolewa kwa Mtendaji wa Serikali za Mitaa ambaye atarekodi kwa
njia ya simu na taarifa hizo zitafika moja kwa moja kwenye Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) ambao wataweka kumbukumbu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mussa Iyombe alisema
kuwa ili kufanikisha uhakiki huo, serikali imetenga Sh bilioni 1.6
wakati wahisani wamechangia Sh bilioni 1.4.
Iyombe
alisema takwimu hizo pia zitaisaidia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA) na Wakala wa Udhamini na Ufilisi (RITA) katika utoaji wa
vitambulisho na hati za kuzaliwa na vifo. Aidha, alisema lengo ni
kuhakikisha kila mtu anatumia kitambulisho kimoja pekee kumtambulisha
kuliko ilivyo sasa kwamba watu wanakuwa na vitambulisho zaidi ya saba.
"Hii
itakuwa dawa ya kuwatambua majambazi, wezi, wahamiaji wa kigeni na hata
watoto wanaozaliwa na vifo. Mtendaji wa mtaa atakuwa anarekodi taarifa
hizo kutoka kwa mkuu wa kaya ambapo ataeleza watoto waliokuwepo,
wapangaji wangapi. Mpangaji pia akitaka kuhama ni lazima aseme anakwenda
wapi ili aweze kupokelewa anakokwenda," alisema Iyombe.
Kwa
mujibu wa Iyombe, awali walikuwa wanatumia madaftari katika kusajili
watu waliopo kwenye vijiji na vitongoji hali ambayo ilikuwa na
changamoto kutokana na watendaji wengine kutojaza taarifa za wakazi wao.
Alisema
kuwa serikali imekuwa ikikosa taarifa muhimu za awali na kuamua kuanza
mfumo huo ambao utafanyika nchi nzima kwa miaka miwili.
Aliongeza
kuwa kwa kushirikiana na Chuo cha Takwimu Kusini mwa Afrika waliamua
kuanza mfumo huo Kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo na kwamba
wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Alisisitiza
kuwa sensa ya mwaka 2022 itatumia taarifa zitakazokusanywa kwa kipindi
cha miaka miwili ijayo ili kuondoa ubabaishaji uliokuwa unafanywa awali.
Pia
alisema kwa sasa nchi inapopatwa na janga lolote hutumia taarifa zisizo
rasmi kwa ajili ya kutoa msaada, hivyo vijiji vingine kuona kuwa
serikali haiwasaidii wanapopatwa na matatizo.
Kwa
upande wake, Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Amina Said alisema
kuwa kabla ya sensa nyingine Tamisemi wawe wamemaliza uhakiki wa watu
kutumia mfumo huo.
Alisema kuwa katika nchi zinazotumia mfumo huo, hakuna sensa kwa kuwa wanazo taarifa sahihi za watu wao.
"Mfumo
huu utaingiza watu wapya na kuwatoa waliokufa ili kufanya makadirio
mazuri yatakayosaidia kuwatambua watu wote ikiwemo wavamizi pia
itapunguza muda wa kupata idadi ya watu," alisema Said.
Pia
alisema kuwa wasimamizi wakubwa wa mfumo huo ni Tamisemi hivyo wananchi
washirikiane na viongozi wao kutoa taarifa sahihi ili kuwatambua na si
kwa nia mbaya.
Hata
hivyo alisema kuwa kupitia mfumo huo itasaidia wanafunzi kuandikishwa
kwenye shule zilizopo maeneo yao kuliko kuandikisha watoto nje ya kata
ya mwanafunzi.
Aliwataka
wanasiasa na viongozi wote watambue na kushiriki katika kuwaelimisha
wananchi na kuwatoa hofu kuhusu mfumo huo ili kutoa huduma bora za
jamii.
Naye,
Diwani wa Kata ya Mapinga Bagamoyo ambaye kata yake imefanyiwa
majaribio, Ibrahim Mbonde alisema kuwa ameandikisha kaya 341 kwa njia ya
kielektroniki na kwamba mfumo umeonesha mafanikio makubwa.
Mbonde
alisema serikali imeondoa gharama za kununua madaftari kwa ajili ya
uhakiki ambavyo vilikuwa havijazwi. Alisema walikuwa wanashindwa kupata
taarifa za watu ikiwemo wajawazito wanaojifungulia nyumbani na wanaokufa
na kusababisha kuwepo kwa takwimu za kukisia.
"Kila
kaya inakuwa na namba yake hivyo mtu anayeenda kuhakiki na kutaja namba
tofauti hutambulika kuwa mdanganyifu. Kwa mfano kwangu watu wapo 23,000
ni lazima tungenunua madaftari mengi, njia hii itasaidia kuleta
maendeleo ya Taifa," alisema Mbonde.
chanzo;mpekuziblog.
Comments