SERIKALI imesema mzabuni aliyetengeneza kivuko cha Mv Dar es Salaam hajalipwa asilimia 10 ya malipo yake kutokana na hitilafu zilizopo katika kivuko hicho.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema juzi bungeni kwamba, mzabuni huyo ametakiwa kukifanyia marekebisho kwa gharama zake kifikie kasi ya knots 20 iliyo katika mkataba badala ya kasi ya knots 14.7 ya sasa.
Kutokana na upungufu huo, mzabuni ambaye ni Kampuni ya MS Johns Gram-Hanssen Bergensgade kutoka Denmark, alifahamishwa na kukubali kufanya marekebisho kwa gharama zake kabla hajalipwa asilimia kumi iliyobaki.
“Mzabuni alifahamishwa juu ya upungufu huo na kukubali kufanya marekebisho kwa gharama zake na mpaka kabla ya kivuko kupokewa na kulipwa asilimia 10 ya malipo ya mwisho na mpaka sasa b hajalipwa kiasi hicho cha fedha hadi atakapokamilisha marekebisho hayo,” alisema.
Alisema kwa sasa mzabuni huyo amepeleka mpango wa marekebisho kufikia mwendo kasi uliokusudiwa na kwamba Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) unapitia mpango huo kujiridhisha. Waziri Mbarawa alisema hayo wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti yake.
Alisema taratibu zote zilipitiwa kununua kivuko hicho.
Alisema katika suala la manunuzi ya kivuko hicho, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupitia ripoti yake, alisema upo upungufu wa ununuzi wa kivuko hicho kwa Sh bil 7.9 kupitia Temesa ambao walikinunua Sh mil 4.98 bila VAT.
Alisema, CAG alieleza kuwa upungufu mwingine uliokuwa kwenye mkataba huo ni kutowasilisha hati ya makabidhiano, baada ya kucheleweshwa kwa siku 14.
Akizungumzia ununuzi, alisema Temesa ilitangaza zabuni na kampuni tano ziliomba na Kampuni ya MS Johns Gram-Hanssen Bergensgade iliyokuwa na gharama nafuu ilikubaliwa kwa Sh bil 7.79.
Awali wakiwasilisha bajeti ya Kambi ya Upinzani bungeni, Msemaji wa kambi wa wizara hiyo ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, James Mbatia alisema kivuko hicho ni jipu lililoiva linalohitaji kutumbuliwa mara moja huku akisisitiza kuwa kilinunuliwa chini ya uongozi wa Rais John Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi.
chanzo;habarileo.
Comments