
Mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu yamesema yanahitaji dola milioni 110 za Marekani ili kuzisaidia nchi za kusini mwa Afrika, zinazokabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula na lishe duni iliyosababishwa na ukame.
Elhadj As-Sy, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu amesema watu zaidi ya milioni 31.6 katika eneo hilo hawapati lishe bora kutokana na ukame.
Amesema yumkini idadi hiyo ikaongezeka hadi watu milioni 49 kufikia mwishoni mwa mwaka huu, iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa.
Kutokana na kutonyesha mvua za kutosha mwaka jana, maeneo mengi ya nchi za Afrika Kusini, Lesotho, Swaziland, Malawi, Msumbiji, Namibia and Zimbabwe yanakabiliwa na ukame na baa la njaa.
Haya yanajiri siku chache baada ya Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) kutangaza kuwa, takribani watu milioni 9 na laki mbili walioko katika eneo la Ziwa Chad ambalo limekuwa uwanja wa jinai zinazofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram wanahitajia misaada ya chakula.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulisema katika ripoti yake kwamba, kutokana na hali mbaya ya hali ya hewa maarufu kwa jina la El-nino, mwaka huu 2016 watu milioni 60 wataongezeka katika idadi ya watu wanaotaabika kwa njaa duniani ambapo nusu ya idadi hiyo wanapatikana barani Afrika.
chanzo;parstoday.
Comments