Shirika la madaktari wasio na mipaka limesimamisha kazi zake katika maeneo ya magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Gazeti la Le Figaro la nchini Ufaransa limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, madaktari hao wamelazimika kusimamisha kazi zao katika maeneo ya magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuanzia jana Alkhamisi baada ya mwenzao mmoja kuuawa katika maeneo hayo.
Shirika hilo linalotoa misaada ya kibinadamu, limesema kuwa, halitaendelea na kazi zake katika maeneo hayo hadi pale wafanyakazi wake watakapodhaminiwa usalama wao.
Kwa mujibu wa shirika hilo, tangu mwaka 2013 wakati ukosefu wa amani ulipoongezeka huko Jamhuri ya Afrika Kati, zaidi ya taasisi 70 za afya zimeharibiwa kikamilifu nchini humo.
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na wale wa Ufaransa wamekuweko nchini humo tangu mwaka 2013 lakini hadi hivi sasa wameshindwa kuleta utulivu na amani katika nchi hiyo iliyokumbwa na mapigano ya kikabila na kidini.
chanzo;parstoday.
Comments