Wanao bagua wananchi kufungiwa Pemba.

Na Shaaban Ali.
Mkuu wa Wilaya ya Wete Rashid Hadidi Rashid amesema  Serikali itaendelea kuzizuia kufanya kazi gari za abiria ambazo zinawabagua wananchi kwa misingi ya kisiasa.

Akizungumza na madereva wa gari zinazofanya kazi katika barabara ya Wete -Mtambwe amesema kwamba mbali za kuzizuia , pia madereva watapokonywa leseni zao pamoja na leseni za njia , kwani zitakuwa zinakwenda  kinyume na taratibu zilizowekwa.

Aidha ameeleza kuwa Serikali iko tayari kuruhusu gari hizo kufanya kazi ya kuchukua abiria , iwapo madereva na matingo watamuhakikishia kwamba hawatawabagua abiria .

Kwa upande wake Nassor Juma Abdalla mkuu wa magari katika Standi ya Wete ,  amewataka madereva kumpa taarifa iwapo kutajitokeza mgogoro wa abiria ili aweze kuchukua hatua za kuwasiliana na Serikali ya Wilaya kwa hatua za kisheria.

Hata hivyo mkuu wa madereva katika katika barabara hiyo  Khamis Seif Khamis amemwahidi Mkuu wa Wilaya kuwa  suala hilo halitajitokeza na atahakikisha kwamba madereva pamoja na matingo wao wanaheshimu masharti ya leseni zao.


Jumla ya gari tatu za abiria katika barabara hiyo zilizuiwa kufanya kazi baada ya kubainika kuwashusha ndani ya gari hizo wananchi ambao ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) 

Comments