Licha ya kuwepo kiwango kikubwa cha uzalishaji wa zao la mwani lakini bado ni changamoto kwa wakulima.
Serikali ya mapinduzi Zanzibar, inaombwa kuandaa mikakati na sera madhubuti itakayosimamia na kuendeleza biashara ya mwani, ili kuwasaidia wakulima wa zao hilo, kujikimu na ukali wa maisha pamoja na kuongeza pato la nchi na taifa kwa ujumla.
Maombi hayo yametolewa na wakulima na wadau mbambali wakiwemo wanafunzi kutoka Chuo cha uongozi wa fedha chwaka, wakati wanafunzi hao, wakiwasilisha ripoti ya utafiti kuhusiana na biashara ya mwani uliofanyika Gombani, Chake Chake Pemba.
Wakati wakiwasilisha ripoti juu ya utafiti huo, wanafunzi hao walisema kuwa,wakulima wengi katika visiwa vya Zanzibar wamekuwa wakijishughulisha katika biashara ya mwani bila ya mafanikio yoyote, kutokana na kukosekana sera madhubuti inayosimamia na kutetea hali zao.
Walisema, pamoja na jitihada wanazofanya wakulima hao, lakini bado serikali inahitajika kuratibu vyema mipango yake, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wa taasisi mbali mbali kwa ajili ya kuwakomboa wakulima, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa litasaididia ongezeko la uchumi wa nchi.
Nd. Said amesema kuwa, kati ya wakuli wa mwani 23,000 Zanzibar, inaonekana kuwa asilimia 77.5 ni akina mama kati yao asilimia 67.1 ni watu wazima wenye umri kati ya miaka 36 hadi miaka 60.
Sambamba na hayo amesema vijana wengi wamejitoa katika biashara hiyo, baada ya kuvunjika moyo kutokana na kipato kidogo kinachozalishwa kulinganisha na gharama na kazi kubwa ya ukuli wa mwani.
Kwa upande wake, mkuu wa Idara ya mazao ya baharini Pemba, Hidaya Khamis Hamad, amesema kuwa, wakulima wa mwani wapatao 16,500 kisiwani pemba, wanaendeleza shughuli zao kwa kutegemea mwani, ambapo kipato chao bado ni kidogo kulinganisha na shughuli wanazozifanya.
Amesema, nimatumaini yao makubwa kuwa, utafiti uliofanya na wanafunzi hao, utasaidia Serikali kwa kiasi kikubwa katika kuandaa sheria zitakazo weza kunyanyua na kulinda hadhi ya wakulima pamoja na wafanyabiashara wa zao la mwani.
Akichangia katika uwasilishaji wa ripoti hiyo, Nd. Salum Mohammed Hamza, kutoka wizara ya biashara, alisema kuwa, pamoja na michangio mengi iliolenga kuandaliwa sera lakini bado kuna haja ya kufuatilia na kujua ni vitu gani vinafanywa kupitia mwani na kuwapa utajiri wakulima wa nchi washirika, ili kuweza kupata wigo badala ya kusafirisha kama ulivyo.
Kwa upande wake, mkulima wa mwani, kutoka Shumba Mjini, Nd. Rashid Omar Matta, alisema kuwa, ni vyema kwa wafanyabiashara kusitisha kusaidia vifaa na badala yake kuwapandishia bei ambayo itawasaidia katika kununua vifaa wenyewe na kukidhi mahitaji ya kifamilia.
Mkutano wa uwasilishaji wa ripoti ya utafiti wa hali ya biashara ya mwani, uliwashirikisha wadau mbali mbali kisiwani Pemba, wakiwemo wafanyabiashara , wakulima, maafisa waserikali pamoja na taasisi binafsi kwa lengo la kuboresha hali ya biashara ya mwani na kusaidia kipato kwa wakulima.
Comments