Chikawe apelekwa Japan, Ma-DC Kinondoni, Musoma wateuliwa.

RAIS John Magufuli amemteua Mathias Chikawe kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan.
Pia Rais Magufuli amemteua Ally Salum Hapi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Halikadhalika, Rais Magufuli amemteua Hamphrey Polepole kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, uteuzi wa Chikawe umeanza Aprili 13, mwaka huu.
Balozi huyo ataapishwa leo. Kabla ya kupangiwa kituo hicho cha kazi, Chikawe aliteuliwa kuwa Balozi Februari 15, mwaka huu.
Aliteuliwa na wenzake wengine wawili, Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa na Waziri katika Serikali katika Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Asha-Rose Migiro na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamiii (NSSF), Dk Ramadhan Dau.
Chikawe aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Nachingwea mkoani Lindi kati ya mwaka 2005 na 2015, na kwa vipindi tofauti katika Serikali ya Awamu ya Nne alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kuhusu mkuu mpya wa Wilaya ya Kinondoni, taarifa ya Ikulu ilisema uteuzi huo umeanza jana Aprili 18, 2016 na Hapi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Paul Makonda aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kuhusu Polepole, taarifa hiyo ya Ikulu ilisemaPolepole anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (mstaafu), Zelothe Steven ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Uteuzi wa Polepole ulianza jana.
chanzo;habarileo.

Comments