Watumishi 680 TRA wanolewa kukusanya kodi.



Zaidi ya wafanyakazi 680 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamepata mafunzo ya ukusanyaji wa kodi katika sekta ya mafuta na gesi, yaliyotolewa na Shirika la Misaada la Kimataifa la Japan (JICA).
Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa TRA, Victor Kimaro, aliysema hayo juzi, wakati wa kumalizika kwa mkataba wa makubaliano wa miaka minne waliongia JICA na Tanzania wenye thamani ya dola za Marekani milioni 3.5 (Zaidi ya Sh. bilioni saba).
Kimaro alisema mafunzo hayo pia yalilenga kujenga uwelewa wa masuala ya ukusanyaji wa kodi, namna ya kutunza kumbukumbu za makusanyo  katika kompyuta na ukusanyaji bora wa kodi katika mafuta na gesi.
“Leo ndiyo tumefikia mwisho wa MoU, lakini kumalizika kwa mkataba huu ndiyo mwanzo wa makubaliano ya mkataba mwingine. Mkataba huu ulianza miaka minne iliyopita,” alisema Kimaro.
Kimaro alisema TRA imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Jeshi la Polisi nchini katika kudhibiti uingizwaji wa bidhaa za magendo mipakani na katika bandari bubu.
Naye Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA), Prof. Isaya Jairo, alisema kwa sasa ITA, mbali na kumalizika kwa mkatana huo, inatafuta wafadhili  watakaosaidia upatikanaji wa vifaa vya kufundishia kama vile kompyuta.
Alisema wakati wa mafunzo hayo, changamoto zilizojitokeza ni pamoja na lugha kutokana na watoa mada kutofahamu vizuri lugha ya Kiingereza.
Mwakilishi wa JICA Tanzania, Toshio Nagase alisema mafunzo waliyoyatoa kwa wafanyakazi wa TRA yatasaidia katika ukusanyaji wa kodi na kukuza uchumi wa nchi.
Alisema Tanzania ni nchi inayoendelea kiuchumi, hivyo kwa mika 10 ijayo ukusanyaji wa kodi utaongezeka maradufu.
chanzo;ippmedia.

Comments