Vituo 21 vya mafuta Moro havijafunga mashine za EFDs.

VITUO vitatu vya mafuta katika Manispaa ya Morogoro, ndivyo vinavyotumia Mashine ya Kodi za Kielektroniki (EFDs) kukusanya mapato ya Serikali. Vituo hivyo ni Oryx kilichopo jirani na Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ; na Puma na Petrol vilivyopo eneo la Msamvu, nje kidogo ya mji.
Vituo hivyo vitatu ni kati ya vituo 24 vya mafuta vilivyopo katika Manispaa ya Morogoro. Hii ina maana vituo 21 bado havijafunga mashine hizo. Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven Kebwe (pichani), amemwagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro, Philip Kimune kuhakikisha vituo vyote vya mafuta, vinatumia EFDs kukusanya mapato ya Serikali.
Dk Kebwe alitoa agizo hilo kwa Meneja huyo wa TRA mkoa, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika vituo vya mafuta vilivyopo Manispaa ya Morogoro. Katika ziara hiyo, ndipo Kebwe alipobaini kuwepo kwa vituo hivyo vitatu tu, vinavyotumia mashine hizo kati ya vituo 24 vilivyopo.
Mkuu huyo wa Mkoa alifanya ziara ya kustukiza katika siku zake za mwanzo wiki iliyopita, baaada ya kuteuliwa kwake kushika wadhifa huo kushika nafasi ya mtangulizi wake, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Dk Rajab Rutengwe.
Katika ziara hiyo ya vituo vya mafuta vilivyopo Manispaa ya Morogoro, Mkuu wa Mkoa alibaini kuwa vingi havitekelezi agizo la Serikali. Kebwe alimwagiza Meneja huyo wa TRA mkoa, kuhakikisha kuwa mashine hizo zinafungwa katika vituo vyote vya mafuta ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanzia Machi 19 hadi Aprili Mosi mwaka huu bila kukosa.
Alisema kuwa agizo hilo lilitolewa na Serikali miezi miwili iliyopita kwa wamiliki wa vituo hivyo. Dk Kebwe alivipongeza vituo vya mafuta vya Oryx, Puma na Petrol, kwa kutumia mashine za EFDs katika kukusanya mapato ya serikali kwa uhakika. Kwa upande wake, Kimune alimuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa suala hilo litafanyiwa kazi mara moja.
chanzo;habarileo.

Comments