Hospitali ya Rufaa Mkoa Kagera kufunga mfumo wa kielektroniki.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, inatarajia kufunga mfumo wa kielektroniki ili kuwezesha mgonjwa yeyote atakayetibiwa kupatiwa risiti ya kimtandao.
 
Akizungumza na Nipashe ofisini kwake, Katibu wa hosptali hiyo, Kilwanira Kiiza, alisema mfumo huo mbali na kuongeza mapato ya serikali, pia utasaidia kuondoa malalamiko ya wagonjwa kwamba wamekuwa wakilipia huduma ambazo hawajapatiwa.
 
Kiiza alisema mashine tano kwa ajili ya kufunga mfumo huo zinatarajiwa kuwasili wiki ijayo na kuwa kupitia mfumo huo dawa ambayo mgonjwa hakupatiwa, hatalipishwa na hakuna fedha za mgonjwa zitakazochukuliwa bila mgonjwa husika kupatiwa huduma.
 
Aliwataka wananchi kuhakikisha wanapewa risiti kulingana na huduma waliyoipata na kuwa mwananchi ambaye hatachukua risiti ya kimfumo, naye atakuwa amechangia kuiibia serikali mapato yake.
 
Alisema mashine hizo zitafungwa katika maeneo mbalimbali ya hospitali ili kuwezesha mgonjwa kupata risiti katika kitengo alikopatiwa huduma.
 
Aliwaomba wananchi kutokubali kuchukua risiti za kuandika kwa mkono.
 
Aidha, aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watendaji wa hosptali hiyo ili kuwawezesha kutoa huduma bora.
chanzo;ippmedia.

Comments