Ushauri huo ulitolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria na Katiba wakati ikichambua mpango na mapendekezo ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria mjini hapa.
Wakati kamati hiyo ikishauri hayo, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi aliiambia kamati kuwa, atalifikisha suala hilo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ili kwa pamoja walishughulikie.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rashid Shangazi akitoa mapendekezo ya kamati kwa wizara hiyo, alisema wanapendekeza sheria hiyo ya elimu itamke kuwa elimu ya sekondari kuwa ya lazima.
“Ndugu yangu Amon Mpanju, (Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo ambaye ana ulemavu wa macho) wakati ule akiinadi Ilani ya CCM alisema elimu ya msingi iwe mpaka sekondari, sasa hili lifanyiwe kazi kisheria,” alishauri Shangazi.
Ijumaa, wakati wa mjadala, Mbunge wa Bahi, Omar Badwel (CCM) akitoa hoja alisema sheria hiyo ya elimu namba 5 inatamka kuwa elimu ya msingi ndiyo ya lazima na haizungumzii kuwa elimu ya sekondari ni ya lazima.
“Sasa hivi serikali inatekeleza elimu bure, lakini lipo tatizo hapa, wapo wazazi pamoja na elimu ya sekodari kuwa bure, hawawapeleki watoto shule na wakifikishwa mahakamani, wanaachiwa maana sheria haijasema kuwa elimu ya sekondari ni lazima, hivyo inakuwa hiari kwa wazazi kumpeleka mtoto ama kuacha,” alifafanua Badwel.
Alishauri elimu ya msingi kuishia sekondari ili wazazi wanaowakatili watoto kuipata elimu hiyo, washitakiwe kwa mujibu wa sheria.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Kabudi alisema, “Tumelichukua hili. Ukweli tujiulize, nini maana ya elimu ya msingi? Elimu ya msingi maana yake kila mtu lazima awe nayo. “Nitamfikishia Waziri wa Elimu (Profesa Ndalichako) ili tuanze mchakato wa kuifikisha elimu ya msingi kidato cha nne,” alisema Profesa Kabudi.
Kwa Tanzania Bara, elimu ya msingi ni ya shule za msingi, lakini Zanzibar inatambua elimu ya msingi mpaka kidato cha pili.
Hoja hiyo iliibuliwa wakati kamati hiyo ikipitia utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2016/17 na mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/18.
chanzo:Habarileo.
Comments