MKOA wa Arusha umepanga kutumia Sh bilioni 12 katika mwaka wa fedha 2016/17, kwa ajili ya sekta ya barabara.
Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Arusha, Johnny Kalupale alisema hayo jana ofisini kwake na kusema kuwa kilometa 104.5 za barabara zinapaswa kukarabatiwa.
Kalupale alisema katika mpango kazi huo, madaraja 10 yatakarabatiwa na utafanyika usanifu wa barabara 33. Alisema pia zitajengwa kilometa mbili za barabara kwa kiwango cha reli.
Meneja huyo alisema Tanroads imejipanga kukarabati barabara za changarawe zenye urefu wa kilometa tano.
Alisema shughuli hiyo itakwenda pamoja na ujenzi wa madaraja 10 ya barabara za mkoa pamoja na usanifu wa barabara kuu zenye kilometa 33.
Akizungumzia mradi wa barabara ya KIA-Mirerani anaogharimu zaidi ya Sh bilioni 32.2, alisema unakwenda vizuri na hadi sasa umetekelezeka kwa asilimia 32.5. Kalupale alisema barabara hiyo yenye kuingizia nchi mamilioni ya fedha kwa biashara ya madini ya tanzanite, itakamilika kama ilivyopangwa Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema kampuni inayojenga mradi huo pamoja na kupata changamoto nyingi katika suala la changarawe inaendelea vizuri kwa kasi ambayo yeye kama msimamizi mkuu wa barabara hiyo anaridhika.
Meneja huyo alisema changarawe ni tatizo kubwa katika mradi huo kwani hazipatikani na zikipatikana wenye maeneo huhitaji gharama kubwa.
chanzo;habarileo.
Comments